Manqoba Mngqithi Yanga
Yanga SC

Manqoba Mngqithi Aweka Mipango Hadharani Yanga SC

Vardo August 29, 2026 10:45 am

KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, ameanza rasmi maandalizi ya kikosi chake kuelekea mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisisitiza umuhimu wa kila mshambuliaji kutumia vyema nafasi anazopata ili kupunguza presha na kuongeza ushindani wa namba ndani ya timu.

Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alifanya mabadiliko ya wachezaji kadhaa ili kuwapa fursa wengi wao kupata dakika za kucheza, hatua aliyoeleza kuwa ni sehemu ya mkakati wake wa maandalizi ya kimataifa.

Mngqithi alieleza kuwa kabla ya kuingia uwanjani, aliwaagiza wachezaji kuhakikisha washambuliaji wote wanapata fursa ya kufunga. Hatua hiyo inalenga kuondoa utegemezi kwa mchezaji mmoja na kusaidia safu ya ushambuliaji kucheza kwa uhuru.

“Niliiambia timu ihakikishe washambuliaji wetu wote wanapata nafasi ya kufunga. Hilo litaondoa presha kwa kila mmoja na kuwafanya wacheze kwa uhuru zaidi uwanjani,” alisema Mngqithi.

Pia alionyesha kufurahishwa na mshambuliaji aliyefanikiwa kucheka na nyavu, akibainisha kuwa mchezaji huyo amekuwa akitengeneza nafasi nzuri kwenye michezo iliyopita lakini alipata changamoto ya makipa wa wapinzani kuokoa michomo yake.

Licha ya kuondoka na pointi tatu, Mngqithi alibainisha kuwa bado hajashiba kiwango cha umaliziaji cha safu yake ya ushambuliaji, kwani timu ilitengeneza nafasi nyingi zaidi zilizostahili mabao.

“Katika soka lazima tukubali matokeo. Kuna wakati unatengeneza nafasi lakini huzitumii zote. Kwa sasa tunafurahia kutokuruhusu bao na kufunga mawili, ingawa mchezo huu ulikuwa na uwezo wa kuzaa zaidi ya mabao saba. Lakini tunashukuru kwa kile tulichopata,” aliongeza.

Mzunguko wa Kikosi (Rotation)

Akizungumzia mabadiliko ya kikosi (rotation), Mngqithi alifafanua kuwa mpango huo unalenga kujiandaa na ratiba ngumu ya mashindano inayowakabili, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga inatarajia kuanza mechi zake za kimataifa ugenini dhidi ya Gaborone United ya Botswana Septemba 5, 2026.

“Nalazimika kufanya mzunguko wa wachezaji kwa sababu tunakaribia mechi za Ligi ya Mabingwa. Lengo langu ni kuona kila mchezaji anakuwa na utulivu na dakika za kutosha ili tuweze kubadilisha kikosi kwenye Ligi Kuu na Kimataifa bila kushusha kiwango,” alisema Mngqithi.

Baraza Afunguka Baada ya Kipigo cha Yanga: Aweka Wazi Tatizo la Pamba Jiji