Nathaniel Chilambo Simba SC vs Azam FC
Azam FC

Chilambo Aapa Azam FC: “Tuko Kwenye Mbio za Ubingwa, Azam Complex Hatuachi Pointi!”

Vardo September 16, 2026 5:59 pm

BEKI wa kulia wa Simba SC, Nathaniel Chilambo, leo anatarajiwa kuwa kwenye wakati wa kipekee atakapovaana na waajiri wake wa zamani, Azam FC, katika mchezo wa Mzizima Derby utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Chilambo, aliyejiunga na Simba katika dirisha kubwa la usajili akitokea Azam FC, anakutana kwa mara ya kwanza na waajiri wake hao wa zamani tangu aondoke, jambo linaloufanya mchezo wa leo kuwa wa hisia na maalum sana kwake.

Presha ya Mzizima Derby na Mbio za Ubingwa

Mbali na kukutana na wachezaji aliowahi kushirikiana nao, Chilambo anafahamu vyema ukubwa wa dabi hii pamoja na presha iliyopo ndani ya kikosi cha Simba, hasa kutokana na umuhimu wa kuvuna pointi tatu ili kuendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Akizungumzia mchezo huo, Chilambo amekiri kuwepo kwa presha kubwa, lakini akasisitiza kuwa lengo lao kuu ni kuhakikisha hawapotezi pointi.

“Presha ipo kwa sababu kwetu sisi tunahitaji matokeo mazuri tu. Hatutaki kupoteza pointi kwa sababu tuko katika mbio za kugombea ubingwa. Katika hatua hii, kila pointi ni muhimu na hatutaki kuchezea fursa yoyote,” alisema Chilambo.

Beki huyo aliongeza kuwa kucheza dabi kubwa kama Mzizima Derby kunawapa wachezaji uzoefu wa ziada wa kukabiliana na ushindani wa kiwango cha juu, huku akibainisha kuwa matokeo chanya ndiyo kipaumbele chao cha kwanza.

Ushindi wa Afrika Wawapa Morali Kubwa

Chilambo ameeleza kuwa ushindi wa hivi karibuni kwenye michuano ya Kimataifa dhidi ya Mighty Wanderers umeongeza kujiamini na morali ya kutosha kikosini kuelekea mpambano wa leo.

“Mchezo wetu uliopita umetupa nguvu na hamasa kubwa. Sisi kama wachezaji tumehamasishana na kukubaliana kufanya kazi kubwa uwanjani. Ili kutwaa ubingwa, lazima tushinde mechi kama hizi,” aliongeza.

Ujumbe Bizwi kwa Mashabiki wa Simba

Akiwazungumzia mashabiki wa Msimbazi, Chilambo amewasifu kwa kujitoa kwao na kuendelea kuwa nguzo muhimu ya timu hata katika nyakati ngumu.

“Mashabiki wa Simba wanajitoa sana na wanaipenda timu yao. Hata mambo yanapokuwa magumu wanaumia kwa sababu wanataka ushindi muda wote. Tunawashukuru sana kwa support yao isiyo na mipaka.

Tunawaomba wajitokeze kwa wingi leo Azam Complex kama walivyofanya mechi iliyopita. Tunawaahidi kupambana mwanzo mwisho ili tuondoke na pointi zote tatu na kuwapa furaha,” alimalizia Chilambo.

Yanga Yatuliza Presha Aziz Ki Kutokosa Kariakoo Dabi Dhidi ya Simba