Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Hatarini Kusimama: Klabu Zaigomea TFF Kisa Ukata!
GIZANI! Hali ya mambo ndani ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) imeingia kwenye utata mzito baada ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo kufikia hatua ya kuomba kusitisha kushiriki. Hatua hii imekuja kufuatia ukata mkali na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kila msimu, huku zikilitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukaa nazo mezani kusaka suluhu ya haraka.
Klabu hizo zimesisitiza kuwa msimamo huo si wa kuikomoa TFF, bali zimechoshwa na mzigo mkubwa wa hasara na madeni yanayozikabili, huku zikilalamikia kutopata msaada wowote wa kifedha wa moja kwa moja kutoka shirikisho hilo kusaidia bajeti zao.
Ada na Gharama Zaongezeka Mara Duafu
Nyaraka mbalimbali kutoka kwa viongozi wa klabu hizo zinaonyesha mchanganuo wa ada ulivyopanda kwa kiwango kikubwa msimu huu:
-
Ada ya Ushiriki wa Ligi: Imepanda kutoka Sh200,000 hadi Sh472,000.
-
Leseni ya Mchezaji wa Ndani: Imepanda kutoka Sh11,800 hadi Sh23,600.
-
Usajili wa Mchezaji wa Kigeni (TFF): Ada imepanda kutoka Sh3.5 milioni msimu uliopita hadi Sh5.9 milioni.
Hali ni mbaya zaidi kwenye usajili wa wachezaji wa kigeni. Ukijumlisha ada ya TFF na gharama za Kibali cha Kufanya Kazi na Makazi (Work & Residence Permit) kinachofikia Sh7 milioni, klabu inalazimika kutumia hadi Sh12.9 milioni kwa mchezaji mmoja tu wa kigeni.
Gharama hizo ni kabla ya kuhesabu mshahara, usafiri, malazi, chakula na bima ya afya inayotakiwa ya Sh150,000 kwa kila mchezaji (sawa na Sh6 milioni kwa kikosi cha wachezaji 40).
Wadau na Makocha Waonyesha Hofu Yao
Akizungumzia kadhia hiyo, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka, amekiri kuwa gharama hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa timu zisizo na uwezo mkubwa wa kifedha.
“Ndio maana hata sisi msimu uliopita tulipitia changamoto ya kushindwa kuwatumia wachezaji wa kigeni. Sababu kubwa ilikuwa ni changamoto ya vibali ambavyo ni gharama kubwa sana kwa hizi timu ndogo,” alisema Chobanka.
Nao baadhi ya wadau wa soka la wanawake nchini wameonyesha kuunga mkono msimamo wa klabu hizo, wakieleza hofu yao kwa timu changa kama Bunda Girls ambazo hazina wafadhili wa kutosha.
“Hivi kwa Sh12 milioni kwa mchezaji mmoja, Bunda Girls watasajili mchezaji wa kigeni kweli? Vibali vinazidi hata ada ya usajili. Pia naiona Ceasiaa ikisubiri tena mpaka mzunguko wa pili au pengine msimu huu isiwatumie kabisa wachezaji wa kigeni,” alieleza mdau mmoja.
Ombi kwa Waziri Paul Makonda
Kutokana na ugumu wa hali hiyo, wadau wameomba kuandikwa kwa barua rasmi kwenda kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ili kuomba afua za serikali.
“Iandikwe barua kumuomba Waziri asaidie kwa nafasi yake maana hali ni mbaya sana. Mpira umekuwa wa gharama na hata vyama vyetu vya mikoa na wilaya vitakufa. Tunaomba na wadau wengine wajitokeze kuwekeza kwenye soka la wanawake maana mchezo huu umekuwa sana,” aliongeza mdau mwingine.
Jitihada za kuwatafuta viongozi wa TFF ili kuzungumzia mgogoro huu na malalamiko ya klabu bado hazijazaa matunda baada ya kutopatikana.