Keletso Makgalwa wa Simba SC akiwa Afrika Kusini wakati wa kambi ya Oktoba 2026
Simba SC

Simba Yafungwa Tena Sauzi, Sekhukhune 2-1 — Barker Ana Wiki Moja Kabla Ya Dabi

admin October 3, 2026 10:20 pm

Simba SC imemaliza kambi yake Afrika Kusini kwa kipigo kingine baada ya kufungwa mabao 2-1 na Sekhukhune United katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Johannesburg, ikiwa ni siku moja tu baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Polokwane City.

Kama Steve Barker alikuwa amekwenda Afrika Kusini kutafuta majibu kabla ya Dabi ya Kariakoo, basi ameondoka na majibu kadhaa lakini pia maswali ambayo lazima ayamalize ndani ya wiki moja. Dabi dhidi ya Yanga itachezwa Jumamosi Oktoba 10 saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Uhuru.

Simba Ilishtukizwa Dakika Ya Pili

Sekhukhune haikusubiri Simba itulie. Dakika ya pili tu Chibuike Ohizu akatumia shambulizi la kushtukiza na kuandika bao la kwanza wakati safu ya ulinzi ya Wekundu bado haijajipanga vizuri.

Simba iliamka baada ya hapo na kuanza kulitafuta lango la wenyeji. Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 40 baada ya Nickson Kibabage kupiga krosi iliyounganishwa vizuri na Elie Mpanzu na kufanya matokeo kuwa 1-1 kabla ya mapumziko.

Sekhukhune Wakapiga La Pili

Kipindi cha pili kilikuwa na mashambulizi ya pande zote, lakini Sekhukhune ndiyo waliopata bao la pili dakika ya 74 baada ya mshambuliaji wao kuwazidi ujanja walinzi wa Simba.

Dakika ya 87 Kelvin Nashon alitikisa nyavu na kwa sekunde chache Simba ikaonekana imepata bao la kusawazisha, lakini mwamuzi akalikataa baada ya kutafsiri kwamba Neo Maema alikuwa amefanya faulo kabla ya mpira kumfikia Nashon.

Kikosi Kilichoanza Simba

Barker alianza na: Abel; Duchu, Nickson Kibabage, Rushine De Reuck, Che Malone Toure; Fabrice Ngoma Kagoma, Guaye, Neo Maema; Elie Mpanzu, Clatous Chama na Oura.

Katika mabadiliko, Semfuko aliingia nafasi ya De Reuck, Nindi akachukua nafasi ya Toure, Jabaar akaingia kwa Kagoma, Bashir kwa Guaye, Mgunda kwa Mpanzu na Makgalwa kwa Oura.

Vipigo Viwili Sauzi, Dabi Inamaanisha Nini?

Matokeo ya kirafiki hayatoi pointi wala hayachukui pointi, kwa hiyo kufungwa Polokwane na Sekhukhune si sababu ya kutangaza hali ya hatari. Lakini namna mabao yalivyopatikana ndiyo sehemu Barker atakayotaka kuisafisha kabla ya kuiona Yanga.

Dhidi ya Sekhukhune Simba ilifungwa ndani ya dakika mbili za mwanzo. Dhidi ya Polokwane ilifungwa dakika ya 89 baada ya kona. Hiyo inaweka mstari chini ya kitu kimoja — concentration mwanzo na mwisho wa mchezo lazima iwe juu zaidi, kwa sababu Dabi inaweza kuamuliwa na sekunde moja ya kusinzia.

Upande mzuri ni kwamba Simba haikukata tamaa baada ya kufungwa mapema. Ilirudi, ikasawazisha kupitia Mpanzu, ikaendelea kutengeneza nafasi na hata ikafunga bao la dakika za mwisho ambalo lilikataliwa. Hiyo reaction ndiyo Barker atataka kuibeba Dar es Salaam.

Barker Ana Wiki Moja Kusafisha Makosa

Kikosi kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam Oktoba 4 na hapo hesabu zote zinahamia kwenye Dabi. Barker sasa ana takribani wiki moja ya kuweka sawa ulinzi, set-pieces, finishing na kuchagua combination atakayoamini inaweza kuanza dhidi ya Yanga.

Simba haijatoka Afrika Kusini na matokeo mazuri kwenye friendlies zake mbili za mwisho, lakini pengine hilo ndilo jambo ambalo kocha alikuwa anahitaji kabla ya Dabi: kuona makosa yote mapema wakati bado ana muda wa kuyarekebisha.

Oktoba 10 hakuna friendly. Hapo kila kosa litakuwa na bei yake.

Soma Hapa: Simba Yafungwa 1-0 Polokwane, Barker Apata Somo Kabla Ya Dabi

Simba Queens Mabingwa Ngao Ya Jamii, Mnunka Aimaliza JKT — Taji La Pili Hilo