Yanga Princess vs Mashujaa Queens
Simba SC

Yanga Princess Yaibuka Mshindi wa Tatu Ngao ya Jamii kwa Penalti | Soka La Bongo

Vardo October 3, 2026 7:21 pm

Kipa wa Yanga Princess, Molly Nabitaka, ameibuka shujaa na kuivusha timu yake kutwaa nafasi ya tatu kwenye michuano ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake baada ya kuifunga Mashujaa Queens kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulianza kwa Mashujaa Queens kuonyesha nia ya kushinda, ambapo dakika ya 45 Maimuna Hamis ‘Mynaco’ aliifungia timu yake bao la kuongoza kwa mpira wa faulo uliokwenda moja kwa moja kimiani na kuifanya Mashujaa kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga Princess ikisukuma mashambulizi mfululizo kusaka bao la kusawazisha. Jitihada hizo zililipa katika dakika ya 59 pale kiungo mshambuliaji raia wa Ethiopia, Mesay Temesgen, alipopiga faulo kali iliyomwacha kipa wa Mashujaa Queens bila la kufanya na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi kipenga cha mwisho.

Mchuano wa Penalti na Ushujaa wa Nabitaka

Baada ya dakika 90 kumalizika bila mshindi, mchezo huo ulilazimika kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo presha ilikuwa kubwa kwa timu zote mbili.

Kwa upande wa Mashujaa Queens, walioweza kucheka na nyavu walikuwa Sabina Mbuga, Neema Paul, Zainab Dudu na Maimuna Hamis ‘Mynaco’. Hata hivyo, mambo yaliwaendea vibaya baada ya kipa Molly Nabitaka kuokoa penalti ya Saada Magere, huku Tabea Munga na Blandina Ambrose wakipiga nje mikwaju yao.

Yanga Princess walionyesha umakini wa hali ya juu ambapo wapigaji wao Mesay Temesgen, Neema Charles, Agnes Pallangyo na Diana Mnally walifunga penalti zao kwa ufundi mkubwa na kuipa timu hiyo ushindi muhimu na kumaliza katika nafasi ya tatu.

Yanga Princess Yaibuka Mshindi wa Tatu Ngao ya Jamii kwa Penalti | Soka La Bongo