Abdulkarim Segeja
Michezo

Abdulkarim Segeja Afunguka Sababu ya Kusaini Miezi 6 Kigamboni United

Vardo October 5, 2026 10:39 am

Mshambuliaji mpya wa Kigamboni United (zamani B19 FC), Abdulkarim Segeja, ameweka wazi mipango na malengo yake makubwa baada ya kujiunga na kikosi hicho kwa mkataba wa muda mfupi wa miezi sita.

Segeja amebainisha kuwa, ingawa amesaini mkataba wa miezi sita pekee, atahakikisha anapigania kwa jasho na damu malengo ya timu hiyo kwa msimu wa 2026-2027 ili kuongeza ushindani wa hali ya juu kwenye ligi.

Akizungumza kuhusu uamuzi wake huo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union na Tanzania Prisons alisema:

“Hii ni nafasi nzuri kwangu ya kuendelea kuonyesha kiwango changu. Kusaini mkataba wa miezi sita haina maana kwamba hatuwezi kukaa chini na kuongeza mwingine zaidi, isipokuwa malengo yangu makuu ni kujipanga upya na kurudi tena kucheza Ligi Kuu Bara.”

Nyota huyo amejiunga na Kigamboni United msimu huu wa 2026-2027 akitokea Coastal Union ya jijini Tanga, klabu ambayo alijiunga nayo kwenye dirisha dogo la usajili Januari 21, 2026, mara baada ya kuachana na maafande wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

Mashabiki wa Kigamboni United wanasubiri kwa hamu kuona jinsi uzoefu wa Segeja kwenye Ligi Kuu utakavyokisaidia kikosi chao kufanya vizuri msimu huu.

Kocha Morocco Afunguka Siri ya Kambi ya TRA United Zanzibar | Ligi Kuu Bara Zari Hassan Afichua Umri Wake Halisi: “Sina Sababu ya Kudanganya”