Tanzania U-23 vs Kenya
Michezo Bongo

Tanzania U-23 Yaondolewa AFCON U-23 Licha ya Kuisambaratisha Kenya 3-1 Uhuru

Vardo October 6, 2026 7:21 pm

Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 (Tanzania U-23) jioni ya leo imeondolewa rasmi katika michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U-23), licha ya kuibuka na ushindi mnene wa mabao 3-1 dhidi ya Kenya katika mechi ya marudiano iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa dakika 90 uliojaa presha kubwa na msisimko wa hali ya juu, ulishuhudia vijana wa Tanzania wakipambana kufa na kupona kusaka ushindi wa tofauti ya mabao matatu ili kufuta matokeo ya mchezo wa kwanza ambapo Tanzania ilipoteza kwa mabao 4-1 nchini Kenya.

Mwanzo wa Kasi na Mabao ya Tanzania

Tangu dakika ya kwanza ya mchezo, Tanzania ilianza kwa kasi ya ajabu na kulishambulia lango la Kenya mfululizo. Jitihada hizo zilizaa matunda mapema baada ya Shekhan Khamis kufunga bao la kwanza kwa kichwa safi na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki waliojitokeza uwanjani.

Ushindi huo wa mapema uliwaongezea kujiamini vijana wa Tanzania, ambapo nyota Selemani Mwalimu alionyesha kiwango cha juu na kufunga bao la pili kwa njia ya penati kabla ya mapumziko.

Kipindi cha pili kilipoanza, Selemani Mwalimu aliendelea kuibeba timu yake mgongoni baada ya kufunga bao lake la pili kwenye mchezo huo (bao la 3 kwa Tanzania) na kuifanya Tanzania kuongoza kwa 3-0. Kimahesabu, matokeo hayo yangeivusha Tanzania moja kwa moja hadi hatua inayofuata kulingana mechi za nyumbani na ugenini.

Kosa Moja Lililigharimu Taifa

Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla baada ya mshambuliaji wa Kenya, Andre Onyango, kunufaika na makosa ya safu ya ulinzi ya Tanzania na kufunga bao pekee la kufutia machozi la Kenya.

Bao hilo la Onyango lilipoteza kabisa matumaini ya Tanzania kufuzu, kwani kulingana na hesabu za matokeo ya aggregate (jumla ya mabao 5-4), Tanzania ilihitaji ushindi usiopungua mabao 3-0 bila kuruhusu bao ili kuwaondoa Kenya na kutinga hatua inayofuata kukutana na Ivory Coast.

Kauli za Makocha na Wachezaji

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, kiungo mshambuliaji wa Tanzania, Mohamed Shilla alisema:

“Tulifanya makosa wenyewe na walimu wametueleza. Tumejifunza kupitia makosa haya na tutapambana tena kwenye mashindano yajayo kuhakikisha tunafanya vizuri.”

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Tanzania, Ahmad Ally alieleza masikitiko yake lakini akapongeza jitihada za vijana wake:

“Tumeshinda mchezo wa leo lakini kwa bahati mbaya hatujafuzu. Wachezaji walipambana kwa nguvu zao zote, lakini ndio hivyo—mchezo wa mpira wa miguu mara zote unaamuliwa na makosa madogo.”

Said Mundi: Maisha ya Ujerumani, Ngumi na Mbinu za Kupambana na Ugumu wa Maisha