Yanga Yamweka Wazi Kocha Mpya, Ali Kamwe Atoa Tamko Zito!
Msemaji wa Klabu ya Young Africans (Yanga), Ali Kamwe, amewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuachana kabisa na suala la kuondoka kwa Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi, na badala yake kuelekeza nguvu zao zote katika kuisapoti timu ili kurejea kwenye reli ya ushindi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa timu hiyo, Kamwe amewatoa hofu mashabiki akisema kuwa ukurasa wa Kocha Mngqithi umefungwa rasmi, na uongozi upo kwenye mchakato wa kufanya tathmini ya kina ili kumpata mrithi sahihi atakayekiongoza kikosi hicho.
“La kocha limeshapita, Manqoba hayupo tena. Kwa sasa tuwape muda uongozi wetu ufanye tathmini ya nani anakuja kuchukua nafasi hiyo,” amesema Kamwe.
Dira ni Mechi dhidi ya Mashujaa FC
Licha ya mchakato wa kumpata kocha mpya kuendelea nyuma ya pazia, Kamwe amesisitiza kuwa ligi haina Likizo na kwamba Yanga haina nafasi ya kuendelea kupoteza pointi kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu.
Ametolea mfano mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC, utakaopigwa Jumanne hii katika Uwanja wa KMC Complex, akisisitiza kuwa ushindi ni lazima.
“Ligi nayo inaendelea. Jumanne tuna mechi ya nyumbani dhidi ya Mashujaa pale Uwanja wa KMC Complex. Hatuwezi kuendelea kuangusha pointi mfululizo, hili halikubaliki,” aliongeza.
Wito kwa Wanayanga: “Jumanne Twendeni KMC Complex”
Ali Kamwe ametumia fursa hiyo kuwaomba Wanayanga kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa nguvu wachezaji, akieleza kuwa mafanikio ya klabu yanatokana na ushirikiano wa karibu kati ya uongozi, benchi la ufundi, wachezaji, na mashabiki.
Aidha, amewakumbusha mashabiki kuwa tiketi za mchezo huo dhidi ya Mashujaa zimeshaanza kuuzwa kupitia mtandao wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akiwataka kuzinunua mapema ili kuepuka usumbufu na kwenda kuishuhudia timu yao ikipambana kusaka pointi tatu muhimu.