Makocha 6 Ligi Kuu Bara Wanaotembea Kwenye Kamba Nyembamba
MATOKEO ya hivi karibuni katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara yameonekana kuwaweka kikaangoni makocha sita kufuatia mwenendo usioridhisha wa timu zao, hali inayoweka vibarua vyao rehani kutokana na presha kubwa ya kukwepa janga la kushuka daraja.
Kupoteza pointi muhimu na kuambulia sare mfululizo kumezifanya timu hizo kusalia kwenye nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi. Hali hii imeongeza joto miongoni mwa mashabiki na viongozi wanaopambana kuhakikisha timu zao hazishuki daraja msimu hii.
Orodha ya makocha walio kwenye presha kubwa inawajumuisha:
-
Fredi Felix ‘Minziro’ (Fountain Gate)
-
Cedrick Kaze (Kagera Sugar)
-
Francis Baraza (Pamba Jiji)
-
Hemed Suleiman ‘Morocco’ (TRA United)
-
Zuberi Katwila (Geita Gold)
-
Salum Mayanga (Mbeya City)
Tathmini ya Mwenendo wa Makocha na Timu Zao
-
Fredi Felix Minziro (Fountain Gate): Ameanza msimu huu akiwa na matokeo kusuasua, akifanikiwa kushinda mchezo mmoja pekee. Fountain Gate ililala bao 1-0 dhidi ya Simba SC na kufikisha michezo nane mfululizo bila ushindi (sare tatu na vipigo vitano), ikiwa mkiani mwa msimamo ikiwa na pointi sita pekee baada ya mechi 10.
-
Cedrick Kaze (Kagera Sugar): Aliyechukua nafasi ya Juma Kaseja ameshinda mechi moja pekee kati ya nne alizoongoza. Kipigo cha 1-0 dhidi ya Coastal Union kilikuwa mchezo wa tatu mfululizo bila ushindi, na kuifanya Kagera Sugar kushikilia nafasi ya 15 ikiwa na pointi sita baada ya mechi 10.
-
Francis Baraza (Pamba Jiji): Kocha huyu raia wa Kenya yupo kwenye hali tete baada ya kuambulia ushindi mmoja pekee katika michezo 10 aliyosimamia msimu huu.
-
Hemed Suleiman ‘Morocco’ (TRA United): Aliyerithi mikoba ya Etienne Ndayiragije ameshinda mchezo mmoja kati ya sita, huku akiambulia sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.
-
Zuberi Katwila (Geita Gold): Aliyeipandisha Geita Gold daraja ameshinda michezo miwili kati ya 10. Sare ya 1-1 ugenini dhidi ya TRA United ilifanya timu hiyo kufikisha mechi saba mfululizo bila ushindi na kujikuta katika nafasi ya 14.
-
Salum Mayanga (Mbeya City): Wawakilishi pekee wa Nyanda za Juu Kusini wapo kwenye kipindi kigumu baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0. Matokeo hayo yanafikisha michezo sita mfululizo bila ushindi (sare mbili na vipigo vinne), wakisalia nafasi ya 11 wakiwa na pointi 10.
Wataalamu Wanasemaje?
Mchambuzi wa soka jijini Mbeya na nyota wa zamani wa Tukuyu Stars na Coastal Union, Charles Makwaza, ameeleza kuwa mapumziko ya kalenda ya FIFA yamechangia kupunguza kasi ya timu hizo.
“Inahitaji juhudi za haraka na za makusudi kutoka kwa viongozi wa timu hizi kukaa na wachezaji ili kutafuta suluhu. Kwa mfano, Mbeya City ndio wawakilishi pekee wa Nyanda za Juu Kusini, hivyo lazima kuwe na jitihada maalum za kujiokoa mapema,” amesisitiza Makwaza.