Ismail Aziz Kader Aibuka Upya Mbeya City, Aatika Vita Dhidi ya Singida Black Stars
BAADA ya kurejea uwanjani akitokea kwenye majeraha ya nyama za paja, kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Ismail Aziz Kader, amesema yupo tayari kuanza upya mbio za Ligi Kuu Bara huku akionesha kuumizwa na matokeo ya kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Azam FC.
Nyota huyo aliyetua kikosini humo msimu huu akitokea Fountain Gate, amecheza michezo mitano pekee kati ya 10 ya Mbeya City kufuatia majeraha hayo yaliyomweka nje ya uwanja kwa muda.
Ismail alikuwa na kiwango bora msimu uliopita akiisaidia Fountain Gate kumaliza salama kwenye Ligi Kuu, ambapo alifunga mabao matano na kutoa asisti tano msimu mzima.
Hadi sasa akiwa na Mbeya City, hajafunga bao lolote zaidi ya kuhusika kwenye asisti moja, jambo linaloongeza presha kikosini katika vita ya kugania namba na kuisaidia timu hiyo kusogea katika nafasi za juu.
Mbeya City iliyoanza msimu vizuri, kwa sasa imeonekana kukata upepo na kushuka hadi nafasi ya 11 ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi tisa. Timu hiyo itakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Novemba 2 kuikaribisha Singida Black Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo ameeleza kuwa hawakufurahishwa na matokeo ya mchezo dhidi ya Azam FC, na kusisitiza kuwa kwa sasa akili na nguvu zote zipo kwenye mechi ijayo dhidi ya Singida Black Stars ili kuhakikisha wanapata pointi tatu.
Amesema baada ya kukosekana uwanjani kwa muda, sasa kazi inaenda kuanza upya na ameahidi kurejesha kasi yake ya msimu uliopita ili kuisaidia timu yake na kujiweka vizuri kwenye ramani ya soka nchini.
“Nashukuru nimerejea uwanjani baada ya kutoonekana kwa muda. Hatuko pazuri sana lakini hatujakata tamaa, tunaweza kubadilika na kufanya vizuri. Kimsingi ni kuendelea kupambana.”
“Ni matokeo tu ya mpira lakini tunajipanga na mchezo ujao. Tutasahihisha makosa yaliyoonekana ili tuweze kushinda na kujitoa nafasi za chini. Tuna ari, nguvu na hamasa kubwa,” alisema Kader.