RASMI: CAF Yazindua Nembo ya AFCON 2027 PAMOJA
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kwa kushirikiana na nchi wenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027—Tanzania, Kenya na Uganda—limezindua rasmi nembo ya AFCON 2027, hatua inayofungua pazia la shamrashamra kuelekea michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika.
Nembo hiyo ya kipekee iliyobuniwa kwa kuzingatia taswira ya ngao, imezinduliwa rasmi leo saa 7:00 mchana, ikiwa zimesalia siku 212 pekee kabla ya kipenga cha kwanza kupulizwa Juni 19, 2027.
Uzinduzi huu ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kihistoria ya michuano itakayofanyika kwa ushirikiano wa mataifa hayo matatu ya Afrika Mashariki chini ya kauli na jina la TotalEnergies CAF AFCON PAMOJA 2027.
Ubunifu wa nembo hii umebebwa na kaulimbiu isemayo: “Kuheshimu historia yetu, kusherehekea utamaduni wetu na kuashiria Afrika ya kesho”, ikilenga kuakisi utambulisho halisi na urithi wa mataifa mwenyeji.
Maana ya Ngao Katika Nembo ya AFCON 2027
Kwa mujibu wa CAF, matumizi ya ngao katika nembo ya AFCON 2027 si ya bahati mbaya, bali yamechaguliwa kimkakati kuwakilisha utambulisho wa Afrika Mashariki, ulinzi, fahari, udugu na umoja wa wana-Afrika Mashariki.
Ngao ni alama adhimu inayopatikana pia katika nembo za taifa za Tanzania, Kenya na Uganda, hivyo kuifanya kuwa kiungo kinachozikutanisha na kuziunganisha nchi hizi tatu.
Umbo la nembo hiyo limeundwa kwa duara mbili zinazokatana kwa usawa, huku likipambwa kwa nakshi za ushanga na michoro inayochochewa na sanaa za asili za ukanda wa Afrika Mashariki. Katikati yake kuna taswira ya Kombe la AFCON lililozungukwa na ramani ya Afrika, likitoa ujumbe wa namna soka linavyounganisha ndoto, tamaduni na mataifa ya bara hili.
Muunganiko wa Rangi za Mataifa Matatu Wenyeji
Katika kuonyesha mshikamano wa wenyeji wote, nembo hiyo imebeba rangi zinazotambulisha bendera za Tanzania, Kenya na Uganda:
-
Sehemu ya Juu: Imepambwa kwa rangi nyekundu na nyeusi.
-
Katikati (Pembeni mwa Kombe): Rangi za kijani na njano zimetumika kunogesha taswira ya kombe.
-
Sehemu ya Chini: Rangi ya bluu imetawala kukamilisha mwonekano wa kuvutia.
Michoro 12 ya Kipekee Kuitambulisha Tanzania, Kenya na Uganda
Mbali na nembo kuu, CAF imezindua pia michoro 12 ya ngao inayotambulisha utamaduni na alama za mataifa hayo matatu kwa mitindo tofauti ya ubunifu:
-
Tanzania: Imetambulishwa kwa mistari ya mshazari inayotokana na muundo wa bendera yake, ikiwakilisha ardhi yenye rutuba na utajiri wa rasilimali za maji.
-
Kenya: Imetumia mistari mipana ya mlalo kuonyesha nguvu, ustahimilivu na urithi wa taifa hilo.
-
Uganda: Imetumia rangi za joto pamoja na taswira ya ndege wake wa taifa, Korongo mwenye Taji (Crested Crane).
Michoro hii itatumika katika kupamba viwanja vyote vitakavyotumika kwenye mashindano hayo, mabango ya barabarani, pamoja na majukwaa mbalimbali ya kidijitali duniani kote.
Jina PAMOJA limechaguliwa mahususi kuonyesha umoja wa Tanzania, Kenya na Uganda, likitumia Kiswahili kama lugha inayowaunganisha wananchi wa ukanda huu katika safari ya kihistoria ya kuandaa AFCON kwa mara ya kwanza kwa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki.