CAF Yampa Shavu Zito Ahmed Arajiga: Ateuliwa Kuchezesha Mechi Kubwa ya Kombe la Shirikisho Algeria!
Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa kimataifa raia wa Tanzania, Ahmed Arajiga, kuchezesha mchezo mkubwa wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF Confederation Cup) utakaowakutanisha miamba ya Algeria, USM Alger, dhidi ya AS Real de Bamako kutoka nchini Mali.
Mchezo huo wa Kundi D unatarajiwa kupigwa Novemba 29, 2026, katika dimba la Stade du 5 Juillet lililopo jijini Algiers, Algeria. Uteuzi huu ni hatua nyingine kubwa kwa Ahmed Arajiga, ambaye ana beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), akiendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika medani ya soka la kimataifa.
Katika mchezo huo wa Novemba 29, Arajiga atakuwa mwamuzi wa kati, huku akisaidiwa na teknolojia ya usaidizi kwa waamuzi (VAR) itakayosimamiwa na mwamuzi kutoka Zimbabwe, Brighton Chimene.
Uteuzi huu umekuja ikiwa ni muda mfupi baada ya Arajiga kuonesha kiwango bora alipochezesha mchezo wa watani wa jadi (Kariakoo Derby) Oktoba 10, 2026, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga SC.
Aidha, Ahmed Arajiga ndiye mwamuzi pekee kutoka Tanzania aliyechaguliwa miongoni mwa waamuzi 35 bora barani Afrika walioweka kambi jijini Cairo, Misri, kuanzia Novemba 18 hadi Novemba 23, 2026. Mafunzo hayo maalum yaliandaliwa na CAF kwa ajili ya kuwaandaa waamuzi kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa 2026/2027.