Swedy Mkwabi Arudi Upya Simba SC! Achukua Fomu ya Uenyekiti Kimyakimya Bila Mbwebwe
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Swedy Mkwabi, amechukua fomu kwa njia ya mtandao kuwania tena nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari 30, 2027.
Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu ya Simba unaendelea katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambapo wanachama wenye sifa wamejitokeza kuomba ridhaa ya kuiongoza klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa watu wa karibu na Mkwabi, kiongozi huyo wa zamani alikamilisha mchakato wa kuchukua fomu jana jioni kwa njia ya mtandao, utaratibu ambao unatambuliwa na kuruhusiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa Nini Hajatokea Hadharani?
Chanzo hicho kimebainisha kuwa Mkwabi hana mpango wa kufika yeye binafsi katika ofisi za TFF kurejesha fomu hiyo, badala yake anatarajia kumtuma mwakilishi wake kesho, Novemba 20, 2026.
“Muda wowote atamtuma mtu kuirudisha fomu hiyo. Hataki mambo mengi wala kusindikizwa na kundi la watu. Nafikiri anapunguza kelele kwa sababu nafasi hiyo amewahi kuiongoza, hivyo hana presha kubwa. Kesho atamtuma mtu makini kuhakikisha fomu inarudishwa na kusainiwa,” kilieleza chanzo hicho.
Kauli ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF
Akizungumzia utaratibu huo wa kuchukua fomu kidijitali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kibamba, amethibitisha kuwa utaratibu huo ni halali.
“Kipengele cha kuchukua fomu kwa njia ya mtandao kipo. Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu linaendelea vizuri, na kila kitu kitakapokamilika tutatoa taarifa rasmi,” alisema Wakili Kibamba.
Historia Fupi ya Mkwabi Ndani ya Simba SC
Hii ni mara ya pili kwa Mkwabi kujitosa katika kinyang’anyiro cha uongozi wa juu wa Simba SC. Mkwabi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Simba mnamo Novemba 2018, lakini alidumu madarakani kwa takribani miezi 10 pekee kabla ya kujiuzulu Septemba 14, 2019.
Katika barua yake ya kujiuzulu aliyoiwasilisha kwa Bodi ya Wakurugenzi wakati huo, alieleza kuwa sababu kuu ni masuala binafsi pamoja na hitaji la kupata muda mwingi zaidi wa kusimamia shughuli zake za kibiashara. Baada ya kuondoka kwake, nafasi hiyo ilikaimiwa na Mwina Kaduguda kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika.
Wanaowania Uenyekiti Hadi Sasa
Kwa sasa, kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Simba SC kinaonekana kushika kasi, ambapo mbali na Swedy Mkwabi, majina mengine yanayotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Geofrey Nyange Kaburu na Anindumi Jonas.