KIKOSI cha mabingwa wa Afrika mashariki na Kati, Azam FC ambao ni watetezi wa kombe la Kagame msimu wa mwaka 2018/19 mambo yao yalikuwa moto kwani wameweza kutwaa makombe matatu kati ya manne ambayo wameshiriki.
Ni kombe moja tu Azam FC wamelikosa msimu huu ambalo ni kombe la Ligi Kuu Bara wameishia nafasi ya tatu huku mabingwa wakiwa ni Simba.
Pia kwenye fainali zote ambazo walikutana na Simba dozi yao ilikuwa ni mabao 2-1 kisha wanatwaa kombe mazima bila huruma.
Mabingwa hao wametwaa kombe la Kombe la Kagame ikiwa ni maa ya pili baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 kwenye fainali iliyochezwa uwanja wa Taifa.
Shaaban Idd Chilunda, alikuwa miongoni mwa waliofunga kwenye mchezo huo wa fainali na bao lingine lilifungwa na Agrey Moris, Chilunda aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao nane kabla ya kutimkia CD Tenerife ya Hispania.
Januari 13 mwaka huu, kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa Kombe la Mapinduzi,ulirejea Azam FC ikiwa inalibeba kwa mara ya tano kihistoria na kuwa timu pekee iliyolitwaa mara nyingi.
Fainali Azam FC iliichapa Simba mabao 2-1, wafungaji kwa matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wakiwa ni Mudathir Yahya na Obrey Chirwa.
Kama ilivyojiwekea malengo ya kurejea kwenye michuano ya Afrika msimu huu, Azam FC imetimiza ndoto hiyo baada ya Juni Mosi mwaka huu kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, ikiichapa Lipuli bao 1-0, lililowekwa kimiani na Chirwa.
Ikiwa inajipanga kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, kumbuka ya kuwa Azam FC imeandika rekodi kwenye kombe hilo la ASFC, baada ya kulitwaa bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa, ikipata cleansheet katika mechi zote.
Ubingwa huo, ulinogeshwa na udhamini wa Kampuni ya gftrucks ambayo iliidhamini Azam FC katika fainali hiyo iliyofanyika Uwanja wa Ilulu, mkoani Lindi.
Kwa sasa kikosi cha Azam FC kipo likizo, na kitaanza rasmi mawindo ya msimu mpya Juni 20 mwaka huu, kikijiandaa na mtihani wa kwanza wa kutetea ubingwa wa michuano ya Kagame Julai mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.