TUMEANZA vibaya michuano ya Afcon mwaka 2019 huku sera yetu ikituambia kwamba ni zamu yetu kufanya makubwa na kufikia malengo kwa mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa nafasi yetu ya kushiriki Afcon imepatikana baada ya kupita miaka 39 hivyo tunapaswa tuwe na uchungu kwa namna moja ama nyingine kwa Taifa letu.
Kwetu sisi kwa sasa lengo letu la kwanza ambalo ni kubwa kwenye mashindano haya ni kujifunza ili kupata uzoefu hasa kwenye michuano hii mikubwa.
Lile la awali tayari tulilikamilisha kwa kiasi kikubwa na lilirejesha furaha kwa mashabiki na taifa kiujumla ambalo lilikuwa ni kufuzu kushiriki michuano hii.
Kwa kuwa tuliwafunga Uganda ambao ni majirani zetu nao pia wameanza vizuri hatuna haja ya kukata tamaa bali tuwatazame wenzetu kama kioo hasa kwenye michuano hii.
Pia tukitaka kujiweka kwenye fungu moja na Uganda msimu huu sio sawa kwani wao hata msimu uliopita walipenya na walishiriki kwenye michuano hii hivyo wao tayari hatua moja walishatuacha.
Msimu uliopita wao waliingia na waliutumia kama sehemu ya kujifunza jambo ambalo limekamilika kwa sasa wanafanya kile ambacho walikifanya msimu uliopita huku wakibebwa na uzoefu ambao wameupata.
Hilo lipo wazi ndio maana wameanza kuonyesha ushindani kwa sasa hasa kwa kuanza kupata matokeo chanya kwenye mchezo wao wa kwanza tofauti na sisi ambao tuliangukia pua.
Kwa sisi tunaanza hatupaswi kuwa na hasira sana ama kutarajia matokeo makubwa ambayo sio rahisi kuyapata kwa haraka kama ambavyo tunafikiria kwa sasa kwenye mashindano haya.
Bado naona wachezaji wanafanya kitu cha kipekee wanajituma uwanjani na kitu cha kipekee kinaonekana hilo wanapaswa pongezi kwani wanajua kwamba wamebeba furaha ya watanzania.
Nidhamu yao inafurahisha na wanafanya kazi kwa kujituma kwa moyo wao wote wakiwa nje ya uwanja na ndani ya uwanja wanastahili pongezi washikilie hapo wasiachie.
Kwa sasa wanachotakiwa kufanya ni kuongeza juhudi zaidi na mbinu mbadala za kupambana wakiwa ndani ya uwanja ili kupata matokeo.
Kwa sasa ninachokiona kinachochangia wao kufeli kushindwa kupata matokeo ni namna kikosi cha Taifa kinavyopangwa kitaalamu na mwalimu wa timu ya Taifa Emmanuel Ammunike.
Sitaki kusema kwamba mwalimu hajui ama hafai hapana ila ni namna ambavyo mipango inakuwa kwa wachezaji ambao tumezoea kuwaona kwa Taifa letu wakicheza.
Mfano mzuri kwenye mchezo uliopita dhidi ya Senegal ambao tulifungwa mabao 2-0 ni namna ambavyo mshambuliaji John Bocco alibadilishiwa majukumu yake kwa kupewa kazi ya kucheza akiwa ni winga wa pembeni huku Simon Msuva yeye akiwa kwenye nafasi ya ushambuliaji.
Aina ya wachezaji na namna ambavyo wanatumika inakuwa ngumu kwao kuweza kutimiza majukumu ukizingatia mbinu ambayo inatumika ni kushambulia kwa kushtukiza jambo ambalo linampa kazi kubwa Msuva.
Ukiangalia mipira mingi inayomkuta Msuva ni ya juu na yeye ni mfupi hivyo inakuwa kazi kubwa kwake kuimudu jambo ambalo linafanya tushindwe kuonyesha makali kwa wapinzani wetu.
Tunajilinda sana tunashindwa kuuchezea mpira tukiwa ndani ya uwanja hii ni mbinu nzuri lakini ina ugumu wake hasa kwa timu ambayo inahitaji kupata uzoefu na kupata matokeo pia.
Pamoja na kujilinda sana tunatakiwa kutumia mbinu ya kushambulia kama ambavyo wapinzani wetu wanakuwa wakifanya tujipe nguvu na mwalimu anapaswa aangalie namna ya kupanga kikosi chake.
Mfano Burundi mchezo wa kwanza walifungwa lakini wanacheza mpira na wanafanya mashambulizi licha ya kwamba nao hawana uzoefu kwenye michuano hii mikubwa Afrika kuna kitu ambacho wao wanacho.
Bado tunanafasi ya kufanya vizuri kwenye michuano hii ambayo wengi wanaitazama kwa ukaribu kutokana na ukubwa wake.
Tuna michezo mingine mkononi hatupaswi kukata tamaa mapema na kwenye mchezo wetu dhidi ya Kenya hapo tunapaswa tubadili mbinu haraka ili tulete ile ladha ya mpira.
Benchi la ufundi ambalo limeongezwa nguvu linapaswa limshauri mwalimu namna ya upangaji kikosi kwa sasa kwa mafanikio ya Taifa.