Home Uncategorized YANGA YASHUSHA MASTAA AS VITA DAR

YANGA YASHUSHA MASTAA AS VITA DAR


YANGA inataka ianze kutesti mitambo yake kuelekea kimataifa na sasa ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na klabu kubwa za DR Congo, AS Vita na TP Mazembe kwa ajili ya kuzileta hapa nchini kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Yanga wamepanga, kurejesha heshima yao kimataifa kwa kufanya usajili wa kisasa utakaoendana na hadhi ya Yanga katika kuhakikisha wanauchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wameukosa misimu miwili mfululizo na watani zao Simba kuuchukua.

Msimu ujao Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo imepangwa kuanza kutimua vumbi Agosti mwaka huu. Wachezaji ambao hadi hivi sasa tayari imewasajili Yanga ni Issa Birigimana ‘Walcott’, Patrick Sibomana (Rwanda), Lamine Moro (Ghana), Maybin Kalengo (Zambia), Farouk Shikhalo (Kenya) na Sadney Urikhob (Namibia) na Abdulaziz Makame (Zanzibar).

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kati ya timu hizo moja itacheza mchezo huo wa kirafiki na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa mara baada ya michuano ya Kombe la Afrika ‘Afcon’ kumalizika Julai mwaka huu na lengo kubwa ni kuwatambulisha wachezaji wake wapya waliowasajili na kuwatumia katika msimu ujao.

Habari zinasema kati ya klabu hizo mbili, AS Vita yenye mastaa kibao ndiyo inapewa nafasi kubwa ya kuletwa na Yanga kutokana na ukaribu uliokuwepo kati ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera na wa AS Vita, Florent Ibenge ambaye ni bosi wake katika Timu ya Taifa ya DR Congo.

Aliongeza kuwa, Yanga imeandaa tamasha jingine la kihistoria baada ya jana Jumamosi la ‘Kubwa Kuliko’, litafuata la ‘Wiki ya Mwananchi’ ambalo litafanyika baada ya Afcon kwa lengo la wachezaji wao waliokuwepo kwenye timu za taifa wawepo kwa lengo la kutambulishwa kwa mashabiki.

“Tumepanga kuileta klabu kubwa Afrika hapa nchini kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki ambao tutautumia kwa ajili ya kuwatambulisha wachezaji wetu wapya na jezi zetu za msimu mpya wa ligi na mashindano ya kimataifa.

“Kati ya klabu hizo kubwa ni AS Vita na Mazembe ambazo tupo kwenye mazungumzo kati ya hizo Vita ndiyo ipo kwenye nafasi nzuri ambayo imeonyesha nia ya kuja nchini kutokana na uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya Zahera na kocha wao ambaye yeye ni kocha mkuu wa DR Congo na yeye (Zahera) ni msaidizi.

“Na mchezo huo utachezwa siku maalum watakayoitangaza Kamati ya Utendaji ya Yanga ambayo tumeiandaa na kuipa jina la ‘Siku ya Mwananchi’, siku hiyo mashabiki watapata nafasi ya kuwaona wachezaji wao wapya,” alisema mtoa taarifa huyo.

Viongozi wa juu wa Yanga Mwenyekiti, Mshindo Msolla na Makamu wake, Fredrick Mwakalebela hawakuwa tayari kufafanua ishu hiyo jana.

CHANZO: CHAMPIONI

SOMA NA HII  MATOKEO YA MECHI ZOTE ZA LEO NDANI YA LIGI KUU BARA