Na Saleh Ally
YANGA imesajili washambulizi wawili wapya, mmoja kutoka Uganda na mwingine nchini Namibia na wote, waliwahi kukataliwa na Simba.
Sadney Urikhob ni raia wa Namibia ambaye aliwahi kuichezea Simba kwa dakika 45 ikiwa ni Kocha Patrick Aussems akitaka kumuona baada ya kufanya naye mazoezi kwa siku mbili.
Urikhob aliichezea Simba kwa muda huo bila ya kufunga bao lakini akaonyesha ni mchezaji ambaye ana kitu fulani kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, mwepesi wa maamuzi na si muoga kuingia kwenye msitu wa mabeki.
Kawaida wachezaji wamekuwa na hofu wanapokwenda katika majaribio au kutaka kuonyesha vitu vingi kwa wakati mmoja, jambo ambalo limekuwa likiwakosesha nafasi ya kufanya vizuri.
Kama umewahi kusikia, wachezaji wengi wamekuwa hawapendi kufanyiwa majaribio kwa kuwa wanaona hawana nguvu ya kutosha kuidhibiti ile hali ya hofu wakati wa majaribio licha ya kwamba wanakuwa na uwezo mkubwa.
Mchezaji mwingine ambaye Simba haikumfanyia majaribio ni Juma Balinya. Huyu ni Mganda ambaye alimaliza msimu akiwa mfungaji bora baada ya kutikisa mabao 19 katika ligi ya nchi hiyo jirani.
Hata hivyo, Balinya hakuwa katika kikosi cha Uganda maarufu kama The Cranes ambacho kiliingia hadi 16 Bora ya michuano ya Afcon. Na mwisho kikawa ndio kikosi bora zaidi kwa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Simba wamesema waliamini hakuwa amefikia viwango ambavyo wanavihitaji na kigezo kimoja ni kwamba Emmanuel Okwi ambaye walikuwa naye ndiye staa wa Uganda akiwa na timu nchini Misri na Balinya hakuwa na nafasi.
Kumsajili Balinya kwao ilikuwa ni kama kujirudisha nyuma. Hivyo wakaamini hakuwa na vigezo lakini mwisho, Yanga wamemchukua.
Ungeweza kusema Simba wangemsajili Balinya kama mchezaji ambaye anakua. Walifanya hivyo kwa Okwi ambaye alitokea Uganda akiwa kinda na si nyota kama sasa. Lakini bado wana uhuru wa kuchagua na kuamua.
Kwa sisi wadau wa soka, hii ni nafasi nzuri sana ya kujifunza na kuangalia katika kila jambo kama Simba walikuwa sahihi au la.
Je, uamuzi wa Yanga kuwachukua wachezaji ambao Simba wanaoshiriki nao ligi moja waliwakataa, walikuwa sahihi au kuna nini kitatokea?
Mfano ikitokea kweli wakawa na kiwango cha chini, mwisho tutajua walipaswa kufanya nini ambacho ni sahihi na hata wao watajifunza kupitia Simba. Lakini wakifanikiwa, halafu walioonekana na Simba kuwa ni bora zaidi wakawa wa kawaida, pia kutakuwa na nafasi ya kujifunza.
Unakumbuka, Tambwe alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa Simba na Yanga wakiwa mabingwa. Simba iliamua kumuacha na kumchukua Emmanuel Okwi aliyekuwa amerejea.
Moja ya sababu zilielezwa na Simba ni kwamba Tambwe ni mchezaji wa kusimama tu na hakuwa na faida na hata mabao aliyofunga ilionekana angeweza kufanya hivyo akiwa Simba tu. Lakini baadaye akiwa Yanga, Tambwe aliendelea kuwa tishio hata kwa Simba ambayo aliifunga mara mbili.
Tambwe akaiongoza Yanga kubeba ubingwa tena akiwa tishio na tegemeo. Hii ikawapa wakati mgumu Simba kutokana na kujitetea muda mwingi.
Leo, Simba wanachotaka ni kupiga hatua na kusajili wachezaji wa kiwango wanachoamini kitawapa nguvu ya kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba hawataki tena kuishia robo fainali, wakishindwa wanataka wasonge nusu au zaidi. Simba wana ndoto kubwa zaidi, ndiyo maana wamebadili mambo mengi zaidi.
Hakuna anayewalaumu wala kuwakataza lakini kujifunza kupitia wao na walichoamua linaweza kuwa jambo zuri ndio maana natanguliza subira, kama watafanikiwa, ni somo, wakishindwa ni somo kupitia kitabu kingine.
Uamuzi wa mtu kawaida huwa ni mafunzo ya kila siku ya maisha. Inapotokea umefanya jambo majibu yake mara zote hutoa mafunzo. Ndio maana Simba kuwaacha kina Urikhob na Balinya huku Yanga wakiwasajili wakati timu zote zipo ligi moja, ni jambo jingine la kujifunza.
Hivyo, bado kuna nafasi ya kujifunza zaidi kupitia Balinya na Urikhob kwamba Simba wamepiga hatua au wanatakiwa kujifunza zaidi. Yanga wanatakiwa kuamini walichofanya au nao wabadilike. Agosti inakaribia, tusubiri.