Home Uncategorized WAKATI UMEFIKA TUMEACHE AMUNIKE AENDE ZAKE SALAMA, TUSONGE

WAKATI UMEFIKA TUMEACHE AMUNIKE AENDE ZAKE SALAMA, TUSONGE




NA SALEH ALLY
MIAKA 39 michuano ya Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon kwetu ilikuwa ni hadithi. 
Safari hii timu yetu ipo hapa jijini Cairo nchini Misri na leo itashuka kucheza mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi.


Suala la kusonga mbele katika hatua ya mtoano linabaki kuwa majaaliwa. Lakini uhalisia ni hivi, timu inashiriki michuano hiyo.


Kwa miaka 39, Tanzania imekuwa ikicheza dhidi ya timu mbalimbali katika hatua ya kufuzu kucheza michuano hiyo au Kombe la Dunia bila ya mafanikio.


Safari hii imecheza na Senegal kutoka Afrika Magharibi katika Afcon, hali kadhalika majirani Kenya na sasa leo Algeria.


Hii ni hatua kubwa sana ambayo kwa mafunzo na kilichoonekana katika Afcon, basi kuna kila sababu ya kuanza kujifunza na kuyafanyia kazi muhimu.
Stars ilitua katika michuano hii ikiamini iko vizuri lakini uhalisia umeonekana kwa kuwa kiwango cha timu yetu kimeonekana si kiwango bora na hakuna anayeweza kupinga.


Swali la kujiuliza, wenye viwango bora huwa wanafanya nini? Baada ya hapo unaanza kufanya kile kilicho sahihi hata kama itakuwa ni kwa miaka.


Haya yatakwenda kwa mipango ya muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha tunafikia katika kile ambacho kinahitajika ili kufikia ubora sahihi unaoweza kuifanya Tanzania kuwa na timu itakayoshindana katika michuano hii.



Wakati tunawaza hayo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linaweza kukubaliana na uamuzi wa kumuachia Kocha Emmanuel Amunike aende zake, lakini kwa heshima.
Nasema kwa heshima kwa kuwa anaingia katika historia ya makocha waliofanya makubwa kwa kuifikisha Tanzania katika michuano ya Afcon mara ya pili ikiwa imekaa nje baada ya miaka 39.


Kumbuka mara ya mwisho kushiriki mwaka 1980 ilikuwa nchini Nigeria na baada ya miaka 39, Mnigeria ndiye ametuvusha huko.


Wako wanapinga, wanasema si yeye. Kulikubali hilo maana yake kulikuwa na njia haramu zilizotupeleka na si kocha. Kama yupo anaweza kulithibitisha hili, basi ajitokeze na kusimama hadharani, aseme.


Mimi Amunike aende zake kwa kuwa ukiangalia tukubali sote, timu yetu haina uwezo mkubwa. Amunike kama kocha hilo ni jukumu lake.


Alitakiwa kuwainua wachezaji na kuwajengea hali ya kujiamini. Kuwa mzuri katika kuinua ari ya mechi na nguvu ya kwenda kushindana.


Hii ni kwa kuwa hali ya kujiamini ya wachezaji katika kikosi chetu haiko juu sana na inatokana na wachezaji wengi kucheza katika ligi ya nyumbani ambayo bado si kubwa au yenye nguvu sana barani Afrika.


Hata wale wanaocheza barani Ulaya au nje ya Tanzania, bado hawajaweza kufikia kucheza katika ligi kubwa zaidi ambazo zingewafanya kujenga hali ya kujiamini zaidi na wangempunguzia kazi yeye Amunike.


Mchungaji anawasoma kondoo wake na anajua njia sahihi ya kuwaongoza kupita hata kama watakuwa ni dhaifu. Hili lilimshinda Amunike.


Nimebahatika kuzungumza naye mara kadhaa, kosa kubwa nimeona analolifanya, ni kuizungumzia sana Barcelona aliyocheza na umuhimu wake kwa taifa la Nigeria.
Amejisahau yeye ni kocha, anapaswa kujishusha. 

Amejisahau yeye ni baba, anapaswa kuwa chini ili kuinuka na wanaye pamoja.


Nguvu nyingi kuonyesha hababaiki, hajali sana na yeye ni mkubwa sana. Hili ni tatizo linalomfanya kutokuwa kocha aliyeiweza meli aliyokuwa anaiongoza.


Kitu kingine, tunaweza kuwa tunamlaumu sana Amunike, huenda naye unapozungumzia ukocha, hapishani sana na wachezaji wetu kwa maana ya kiwango cha michuano ya Afcon.


Kama mchezaji kweli alikuwa bora sana lakini kama kocha naye ni mchanga. Inawezekana alijitahidi kadiri ya uwezo wake, lakini mambo yakawa ya “mustach”.


Kila jambo, lina hatua. Alipotufikisha yeye, tumpe heshima yake, tutafute mwingine anayetutoa hapa kusonga mbele na lazima awe wa viwango vya Afcon ili kutengeneza kitu tofauti kulingana na tuendako.
SOMA NA HII  MCHUNGAJI MASHIMO, MANARA HAPATOSHI!