Mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya KMC FC dhidi ya AS Kigalo kutoka Rwanda imemalizika kwa wenyeji kukubali kichapo cha mabao 2-1.
Mechi hiyo ya mkondo wa pili imefanyika jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Taifa huku ikishuhudiwa na watazamaji wachache waliojitokeza leo ndani ya dimba hilo.
Walikuwa ni AS Kigali walioanza kupata bao la kwanza kupitia kwa Rashid Kalisa katika dakika ya 29 ya mchezo baada ya kupata pasi safi kutoka kwa mchezaji mwenzake kulia mwa uwanja na kupasia kambani mpira ambao ulimzidi kasi kipa Juma Kaseja.
Bao hilo moja lilidumu mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika AS Kigali wakiwa mbele kwa 1-0.
Kipindi cha pili kilianza tena kwa timu kushambuliana kwa zamu huku KMC wakionesha jitihada za kupata bao lakini kibao kilizidi kuwageukia kwa AS Kigali kuongeza la pili kupitia kwa Eric Nsabimana kwenye dakika ya 64.
Bao hilo lilidumu mpaka dakika ya 87 ambapo KMC walikuja kupata la kufutia machozi kwa njia ya penati iliyopigwa na Suleiman Ndikumana kufuatia mchezaji wa AS Kigali kuunawa mpira uliokuwa eneo la hatari.
Matokeo haya yanaiondoa KMC iliyopata nafasi kwa mara ya kwanza kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakati AS Kigali ikiendelea na mashindano.
Imeandaliwa na George Mganga