Home Uncategorized BAADA YA UD SONGO, BASI VIZURI MUONYESHE HESHIMA KWA JOHN BOCCO….

BAADA YA UD SONGO, BASI VIZURI MUONYESHE HESHIMA KWA JOHN BOCCO….



Na Saleh Ally
MATATIZO ukiyachukulia chanya, yanafundisha. Lakini kila tatizo ukiamini lipo kukuangamiza, basi utaangamia kweli.
Simba waliingia uwanjani kuwavaa UD Songo katika mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiamini wao ni kiboko na Uwanja wa Taifa ni machinjioni, mwisho wakaondoka uwanjani hapo na majonzi.


Hili ni sehemu ya funzo na kitaalamu, mambo hayaendi kishabiki. Ukiangalia katika mechi hiyo ya pili ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya timu hiyo ya Msumbiji, hakika Simba walionyesha soka safi dhidi ya wapinzani bora.


Wakati wakipambana na UD Songo, kama uliangalia mechi hiyo, kukosekana kwa nahodha wao John Raphael Bocco ndiyo kulionekana kuwa tatizo namba moja.



Kukosekana kwa Bocco kuliwafanya mabeki wa UD Songo kucheza kwa raha kwa kuwa kulikosekana kwa mambo matatu makubwa.


Presha:
Bocco ni mchezaji mwenye presha kubwa hasa Simba inapokuwa inatafuta mpira. Anapokwenda kukaba ni msumbufu ambaye anapambana vilivyo na kuwapa presha kubwa mabeki.


Ukabaji wake haumpi nafasi beki kutulia na mpira muda wote bila ya kuwa na hofu. Lakini mara kadhaa, mabeki wanaohofia kuumia kutokana na kashkash za Bocco.
Siku hiyo alipokuwepo Cleotus Chama ambaye alicheza vizuri lakini unaona, mabadiliko ya namba ya Bocco, kuliisumbua Simba.


Meddie Kagere alishindwa kupata mipira kwa ulaini baada ya kukosa purukushani za  Bocco.



Vichwa:
Angalia, Simba walipiga krosi nyingi sana wakati wakishambulia lakini ziliishia katika vichwa vya viungo wa UD Songo.


Mfano baada ya presha kubwa kutoka kwa Simba, kocha wao aliamua kuongeza beki mwingine wa kati na kuifanya UD Songo kucheza na mabeki watatu wa kati na kiungo mmoja mkabaji.


Kama Bocco angekuwa ndani, lazima angewapa shida ya kupiga mipira hiyo lakini purukushani zake lazima wasingekuwa na amani kama ilivyokuwa siku ile.


Uamuzi:
Bocco ana nguvu, anasababisha hiyo hofu, anatengeneza wepesi kwa Kagere lakini uamuzi wake wa kuibeba timu anapoona kuna ugumu.



Ana uwezo wa kufosi kama mshambuliaji na hatabiriki, anatoa pasi ya mwisho au anafunga na mechi mbili kubwa na ngumu za Simba msimu uliopita, dhidi ya Yanga, dhidi ya Al Ahly badala ya kuwa mfungaji, alitoa pasi za mwisho.


Hii inatosha kutoa heshima kwa Bocco na kuacha kuamini ni mchezaji wa kawaida kama ambavyo mashabiki wengi mitandaoni waliamini kukosekana kwake katika mechi hiyo dhidi ya UD Songo ilikuwa sahihi.


Inawezekana Bocco, tunamchukulia poa, lakini tupime rekodi zake. Zina ubora wa juu na wageni wengi hawajawahi kuifikia na ukubwa wa rekodi hizo zimejengwa akiwa Azam FC na si Simba au Yanga.


Tusimdharau kwa kuwa ni Mtanzania. Bocco ni mkubwa katika mpira wa Tanzania na mfano wa kuigwa kwa kuwa hajawahi kuangushwa na mafanikio au ukubwa wake.
Aina yake ni kati ya wachezaji wanaohitajika Simba na Tanzania. Tusimchukulie poa kiasi cha kumuona kuwa yupo tu.


SOMA NA HII  YANGA WAMKATAA MWINYI ZAHERA, AWASEMA MOLINGA NI DENSA WA FALLY IPUPA - VIDEO