JOHN Bocco nahodha wa timu ya Simba jana amekiongoza kikosi chake kulipa kisasi cha kuchapwa bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi uliopigwa Zanzibar kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Simba iliyo chini ya Mblegji, Sven Vandnbroeck ilingia uwanjani na kucheza kwa presha kubwa kutokana na kumbukumbu za kichapo walichokipata mbele ya JKT Tanzania kwa kuchapwa bao 1-0 mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru.
Mtibwa Sugar hawakuanza kinyonge kwani dakika ya saba Haruna Chanongo aliachia shuti ambalo lilipaa juu kidogo na dakika ya tisa Stamili Mbonde aliachia shuti akiwa nje ya 18 liliokolewa na Manula.
Iliwachukua dakika 45 kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Bocco ambaye alitumia juhudi binafsi kuwakwepa mabeki wa Mtibwa Sugar kwa pasi ya Meddie Kagere ambaye ni kinara wa kutupia ndani ya ligi akiwa na mabao 12.
Mpaka muda wa mapumziko Simba ilikuwa inaongoza kwa bao moja na waliporejea kipindi cha pili waliongeza kasi ya ushambulizi na dakika ya 46 Pascal Wawa ilibaki kidogo aandike bao la pili kwa shuti kali akiwa nje ya 18 ila uimara wa Shaaban Kado uliiokoa shuti hilo na dakika moja mbele Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alifunga bao la pili akiwa nje ya 18 kwa kuachia shuti kali.
Bao la tatu lilifungwa na Hassan Dilunga dakika ya 59 kwa pasi aliyorejeshewa na Bocco baada ya kugongeana kuliandama lango la Kado na lilizama kimiani jumla huku Kado akiwa hana la kufanya.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 53 ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza jumla ya mechi 21.