Home Uncategorized TUACHANE NA UPUUZI WA MBONA, KAMA NI KOSA MORRISON, AADHIBIWE NA YANGA...

TUACHANE NA UPUUZI WA MBONA, KAMA NI KOSA MORRISON, AADHIBIWE NA YANGA IANZE…




Na Saleh Ally

KADIRI unavyokubali kujifunza ndivyo unazidi kuyajua mambo mbalimbali kuhusiana na vitu tofauti. Lakini kila unavyojidai au kujiona ni mjuaji, ndivyo mambo mengi yanakupita na unaendelea kubaki na yaleyale uliyoyazoea.


Mimi kawaida nimekubali kujifunza, cha kwanza ninaamini kila mwanadamu hujifunza tokea anaanza kutambua vitu hadi mwisho wa maisha yake bila ya kujali umri aliofikia kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.


Wakati nikiwa nazungumza na mchezaji mmoja wa Tanzania anayecheza nje ya nchi yetu, akanieleza namna ambavyo wao hukatwa mishahara kila wanapopata kadi za njano. Hili jambo lilinishangaza sana, nikajaribu kufanya mawasiliano na baadhi ya wachezaji ninaofahamiana nao ambao waliwahi kucheza Ulaya na ambao wanacheza, wakanieleza jambo hilo.

Wakati nilipokaribishwa katika klabu ya Everton kwa ajili ya mahojiano ya ana kwa ana na wachezaji wao wawili pamoja na kocha pale jijini Liverpool, England. Nikauliza tena kuhusiana na kadi, nikafafanuliwa kuwa kadi ni uzembe na njano na nyekundu zinapishana kwa kiwango cha makato ya fedha.

Kitaalamu kwa maana ya kufuata weledi, kupata kadi ni uzembe kwa maana haukuwa makini au ulichelewa kufanya jambo kwa usahihi, hivyo unapojaribu kulirekebisha bila kuwa makini, utapata kadi. Kupata kadi ni kuipunguzia timu machaguo ya kumtumia nani inayemtaka.

Kuipunguzia klabu wigo mpana wa kuchagua kama ilivyosajili, basi na mchezaji naye unastahili adhabu ili kukuongezea umakini na sehemu nzuri zaidi ya kumgusa mchezaji ni katika malipo yake.

Nidhamu ni jambo muhimu sana pia hata kwa heshima ya klabu. Ndio maana kuna adhabu za kuchelewa kufika kwenye chakula, kuchelewa mazoezini, kuchelewa kupanda kwenye basi na kadhalika. Yote hii ni kutaka kuweka usahihi, kuongeza umakini na kudumisha weledi.

Nimeanza kidogo na elimu ambayo na mimi katika kutembea kwangu nilijifunza kama, ukiikubali sawa, ukiona haifai kama unajua sana, pia sawa.

Nilicholenga leo ni kuuambia uongozi wa Yanga kuwa mfano kuhusiana na mchezaji wake Bernard Morrison raia wa Ghana ambaye aliamua kumpiga kiwiko Jeremiah Juma wa Prisons akiwa anakunywa maji karibu kabisa na daktari na wachezaji wengine.

Mwamuzi wa mchezo huo alikuwepo, sijui kama kweli hakuona lakini Morrison aliamua kumpiga kiwiko mchezaji huyo wa Prisons wakiwa hawawanii mpira au chochote kile.

Bahati mbaya au kinachoshangaza, wachezaji hao walikuwa wakinywa maji pamoja, hali inayoonyesha uhusiano mzuri wa kimichezo.

Vipi huyu Morrison ambaye ulitarajia kuona huenda amezongwa na beki au mchezaji wa upinzani hadi akaingia jazba na kufanya kitu kisicho sahihi? Ajabu hakuwa amesukumwa na hakukuwa na mvutano na hapo unajiuliza, huyu Morrison aliyecheza hadi katika timu kubwa kama Orlando Pirates hajui kuhusiana na picha za runinga, au alidhani Tanzania ni kijijini?

Morrison alipaswa kuwa mfano zaidi kuliko kufanya upuuzi unaoashiria kuna walakini ndani yake, ndiyo maana timu kubwa kadhaa zimeshindwa kudumu naye. Maana yake, bado hajafungua makucha huenda kuna siku ataanza kuwasumbua hata hao Yanga.

Watanzania au mashabiki kadhaa wamekuwa wakilalama Morrison kukosolewa, wengine wakisema mbona Pascal Wawa aliwahi kufanya, mara fulani alifanya hamkusema. 

Mbona katika ujinga, haina msaada na mpira wetu. Tuendelee na mbona, lakini tujiulize, mwisho wa upuuzi wa namna hii ni lini? Nini tofauti ya Ligi Kuu Bara na mchangani?

Shida kubwa wapenda mpira wa Tanzania ni wasahaulifu sana, pia ni wavivu kujikumbusha hata kidogo. 

Ishu ya Wawa tulisema, haswa mimi nilisisitiza na kueleza upuuzi alioufanya Wawa. Wako walioiunga mkono Simba wakaniona ni adui, wakanisakama kwa maneno, jambo ambalo huwa halinipi shida hata kidogo.

Vizuri tuonyeshe weledi, lazima Watanzania tukatae haya mambo. Tunahitaji wachezaji wa kigeni ambao watakuja nchini kwetu kuchuma wakiwa na ubora unaoweza kuwa chachu ya kuwaamsha wachezaji wazalendo na kujituma ikiwezekana siku moja nao waende wakacheze nje ya Tanzania wakiwa mfano mzuri kwa nidhamu na utendaji.

Aina ya mambo haya ya kina Morrison hapana, ushabiki wa kukubali mchezaji amuumize mwenzake eti kwa kuwa unaishabikia timu hiyo ni kuonyesha kutojitambua bila ya kujua.

Yanga inapaswa kumpa adhabu Morrison, kwa kuwa kama atasimamishwa mfano mechi tatu, hasara inapata Yanga kwa kuwa itamlipa mshahara wake wote wa Februari na posho zote.

Jiulize, Yanga ilimsajili Morrison kucheza mpira au kupiga watu? Kama amekuja nchini kucheza mpira, vipi apige wenzake namna ile.

Hatuwezi kukubali mambo mabaya kwa mifano mibaya. Wote wenye tabia kama hizo za Morrison, wachukuliwe hatua. Tuache kuwa watumwa wa mabaya kwa sababu ya mapenzi, tusikubali kusherekea maumivu yaliyo nje ya misingi ya mpira tukasema tunashangilia mpira.

Haya matatu ni muhimu, Yanga imchukulie hatua Morrison, Bodi ya Ligi Tanzania ichukue hatua na tatu, Morrison aombe radhi kwa jambo la kipuuzi alilofanya.



SOMA NA HII  MUKOKO: NINA MKATABA NA YANGA