Home Uncategorized ANKO MWAKYEMBE KAPISHANA NA DUA YETU YA KUTAKA MAPROO WOTE FIRST ELEVEN...

ANKO MWAKYEMBE KAPISHANA NA DUA YETU YA KUTAKA MAPROO WOTE FIRST ELEVEN STARS

NA SALEH ALLY
NDIO raha kwa kuwa kila mmoja anaweza kuwa huru kutoa maoni anayoona ni sahihi. Hii ndio raha ya Tanzania na hasa katika michezo, kikubwa una ambalo unaona sahihi hata kama litakuwa si sahihi.
BIla shaka Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alikuwa na nia nzuri kabisa kuhusiana na kutaka wachezaji wanaocheza nyumbani kupewa nafasi badala ya wale tu wanaocheza nje ya Tanzania.
Dk Mwakyembe kama mzazi anaona kama vipaji vya wale wa hapa nyumbani ni kama vinauwawa, hivyo anataka wapate nafasi badala ya kuangaliwa wale wanaocheza nje tu ya Tanzania.
Haya ni maoni yake ambayo kimpangilio, analenga kuokoa upande mmoja anaoamini unakandamizwa. Kwa watu wa mpira, dua iko tofauti kabisa tena kwa miaka nenda rudi, tunataka wachezaji wengi zaidi wanaocheza nje, ikiwezekana namba moja hadi 11, yaani First Eleven na hata benchi wawe wanatokea nje kwa maana ya England, Ufaransa, Hispania, Ujerumani pia nchi nyingine za Afrika ikiwezekana Misri, Afrika Kusini, Morocco, Ageria na kwingineko.
Tunataka timu imara ya taifa, tunataka wachezaji ambao watakuwa wamepikwa vizuri katika timu na ligi imara watuokoe ili tuweze kusonga mbele zaidi.
Wakati wa michuano ya Afcon ambayo Taifa Stars ilikuwa imerejea baada ya miaka zaidi ya 20, tuliona namna wachezaji wetu walivyokuwa wakibabaisha, walivyokuwa waoga, walivyokuwa hawajiamini na hii ilichangiwa na wengi wao kuwa wanacheza nyumbani pekee.
Ungeweza kusema kuna timu zina wachezaji wa nyumbani wanaofanya vizuri lakini na ligi zao zina ubora wa juu kabisa ukilinganisha na ligi yetu hii. Maana yake, bado tunahitaji Watanzania wengi wakacheze nje ili kuleta mabadiliko katika mpira wetu tukianzia na Taifa Stars.
Mfano mzuri, Shirikisho la Soka Afrika (Caf) liliona jambo alilolisema Mwakyembe na ndio chanzo cha kuanzishwa kwa Chan lakini pia tuzo za wachezaji wa Afrika wanaocheza barani Afrika.
Kuanzishwa kwa michuano hiyo ambayo safari hii tutashiriki kwa mara ya pili baada ya kushiriki kule nchini Ivory Coast, maana yake wachezaji wanaocheza katika ligi za nyumbani, wapate nafasi.
Caf wamelishindwa hili kwa kuwa wameona timu zote zilizopiga hatua katika Afcon, zina wachezaji wanaotokea nje ya nchi zao.
Misri walijaribu kwa kiasi kikubwa na wakafanikiwa wakati wa kizazi cha akina Mohamed Aboutrika, lakini baadaye wameshindwa na leo wanaowategemea akina Mohamed Salah ni nyota barani Ulaya na wana mafanikio makubwa zaidi nje ya Misri.
Vipi sisi peke yetu tupishane na wenzetu wote Afrika nzima, wao wanakwenda Kaskazini na sisi turejee Kusini, haitawezekana!
Unaona kuna tuzo za Afrika kwa wachezaji wanaocheza nyumbani. Sisi Tanzania tunaweza kuwa mfano mzuri wa tuzo hizo. Mbwana Samatta alishinda tuzo hiyo wakati ile kubwa akiichukua Pierre-Emerick Aubameyang, wakati huo alikuwa akiichezea Borussia Dortmund ya Ujerumani na si timu yoyote ya kwao Gabon.
Hata Samatta wakati akishinda tuzo ile ambayo kwa pamoja tuliishangilia sana, alikuwa hachezi Tanzania badala yake alikuwa anaitumikia TP Mazembe ya DR Congo ambako alipatia mafanikio hayo.
Litakuwa jambo zuri sana kama tukiacha kuwaambia wachezaji maneno yanayowadekeza na kuanza kuhisi kama kuna ambao wanapendelewa.
Badala yake wajitume, wapambane na wengi wao kutoka nje ya nchi ambako watajiimarisha zaidi. Walioamua kubaki ndani, basi haina shida, tutawatumia katika Chan kwa kuwa ni michuano mikubwa pia ya Afrika na kwa timu za taifa ni namba mbili baada ya Afcon.
Ukiona unapenda Afcon na mafanikio zaidi, nenda kacheze nje ya Tanzania na baadaye uwe msaada kwa taifa lako.
Tukubali, Anko Mwakyembe alikuwa akitoa maoni yake na kupishana maoni si jambo baya lakini ukweli ndio utabaki kuwa mwongozo sahihi.

SOMA NA HII  ZFF YAFAFANUA JUU YA WACHEZAJI KUONGEZWA, VIINGILIO YANGA V SIMBA BEI JUU