Home Uncategorized UNAIONA FILAMU YA KIFO CHA SINGIDA UNITED ILIVYOANDALIWA NA SASA NI WAKATI...

UNAIONA FILAMU YA KIFO CHA SINGIDA UNITED ILIVYOANDALIWA NA SASA NI WAKATI MWAFAKA WA KUMALIZIA KUSHUHUDIA




Na Saleh Ally
KABLA ya mechi ya jana dhidi ya Alliance, Singida United ilikuwa na pointi 11 mkiani mwa Ligi Kuu Bara na huenda ikabaki hapo hadi mwisho wa ligi.

Singida United, ndio inayoburuza mkia na inaonekana bila ya ubishi kuwa tayari wamekubali ‘kufa’ na wanachosubiri kwa sasa ni muda tu ili uamuzi ufikiwe. Hii maana yake kuwa haiwezekani kabisa kwa wao kubaki Ligi Kuu Bara.

Huenda wakawa wanasubiri miujiza, jambo ambalo litakuwa gumu kwa kuwa wanataka kukomboka kwa kufanya yaliyo sahihi na isingetakiwa yafanyike sasa, badala yake miezi mitano iliyopita. Kwa kifupi Singida United kwa sasa tayari wamechelewa, hawana nafasi.

Ukiangalia pointi walizonazo kujikomboa angalau washinde mechi 10 lakini kwa sasa wana mechi 23 walizocheza kabla ya mechi ya jana na walikuwa wameshinda mechi mbili tu, wamepoteza 16 ikiwa ndio timu iliyopoteza mechi nyingi zaidi kuliko nyingine zote katika ligi hiyo.

Wamefungwa mabao 35 na kufunga 12 pekee jambo ambalo unaona kabisa kwa sasa hakuna dalili za wao kuamka tena na kusema wanaweza kujiokoa wasiteremke daraja.

Walikuwa na wachezaji chipukizi, walianza kama mfumo wao mpya wa maisha mapya katika msimu wa 2019/20. Uhalisia ni kwamba hawakuwa na fedha tena za kusajili wachezaji wa bei mbaya kama ilivyokuwa miaka miwili nyuma. Lakini kiungwana, wakachagua njia nzuri ya kuzungumzia.

Baada ya kuona mambo yanakwenda vibaya, wakati wa usajili wa dirisha dogo, wakaamua kuwarudisha wachezaji wakongwe ambao karibu kila timu tayari walishachoka zao na walikuwa wanakwenda kustaafu. Wakasema wameona vijana pekee “ngoma hailali”, hivyo wanataka wakongwe kwa ajili ya kuwaokoa.

Tumeona, mambo yamekwenda mbiombio kwao, baada ya hapo ushindi wao umekuwa sare zaidi wameendelea kuambulia vipigo mfululizo na hivi karibuni wameanza kusambaratika.

Kuna taarifa hali ya kifedha imezidi kuwa mbaya hadi imefikia baadhi ya wachezaji wakongwe wameamua zao kuondoka kambini na kurejea jijini Dar es Salaam ambako kuna makazi yao.

 Wakati mwingine hauwezi kuamini kuwa hii ni ile Singida United iliyokuwa ikitamba chini ya Kocha Hans Van der Pluijm. Ilifikia hadi kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho ikionekana imara hasa.

Wakati ikifanya hivyo, ilionekana ni timu kubwa sana na wakati mwingine hadi viongozi wake wakatamani kuwekwa katika daraja la Simba na Yanga.

Waliona wanabaguliwa au kushushwa kila walipoonekana hawako katika daraja la timu kubwa, maarufu, inayokubalika na kuheshimika sana.

Kibaya zaidi, hakukuwa na mipango madhubuti ya kuifanya timu hiyo kuwa na mwendelezo. Mipango yake ilikuwa ni ya kisiasa ndio maana unaona leo inadondoka ikiwa haina wa kuisaidia zaidi ya wachache ambao walianza nayo akiwemo Mwigulu Nchemba.

Huenda Mwigulu ni siasa na mapenzi ya dhati lakini wengi wamekimbia na yale mambo ya Singida nyumbani kwa sasa hayaonekani tena kwa kuwa timu hiyo katika kipindi hiki haiwezi kuwasaidia lolote.

Mara nyingi mapenzi ya kisiasa ni ya kinafiki. Bahati mbaya zaidi timu hiyo haikuwa na mipango ya muda mrefu zaidi ya ile ya muda mfupi, sasa inakufa taratibu bila ya muokozi.

Hakuna ubishi, Singida United inakwenda kuteremka, hakuna ubishi wa kuikomboa wameweka mikono nyuma na kinachobaki ni kuomba dua, jambo ambalo linapaswa kuwa funzo kwetu kwamba ikiwezekana, mipango kwa ajili ya kufanya kitu cha muda mrefu ni bora zaidi badala ya kuparamia ukubwa wa haraka, mbwembwe kibao za basi la kisasa, makocha wa bei mbaya, wachezaji rundo wa kimataifa na leo ni hadithi nyingine kabisa, wachezaji hawana hata fedha ya kula na wanaishi Guest House! Kama ni filamu, steringi kafa mwishoni.
SOMA NA HII  ZAHERA AANZA NYODO YANGA