KOCHA wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa kama kweli klabu hiyo inataka kumrejesha mshambuliaji wao wa zamani, Heritier Makambo, anayekipiga Horoya ya Guinea kwa sasa, wafanye hivyo haraka ila wawe na uhakika wa kumlipa mshahara mzuri.
Zahera ambaye inaaminika kuwa ndiye Meneja wa mchezaji huyo, amesema kwake yeye haoni tatizo la Makambo kurudi Yanga baada ya klabu hiyo kuonyesha nia ya kufanya hivyo kwa kuwa nyota huyo alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga na itakuwa vizuri kama akirejea sehemu ambayo aliishi kama nyumbani.
Uongozi wa Klabu ya Yanga, ulithibitisha kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael, ameagiza kusajiliwa kwa wachezaji wanne wa kigeni, ambao ni mshambuliaji mmoja, winga, kiungo wa kati na beki mmoja, ambapo tayari GSM wameshaanza kufanyia kazi ishu hiyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema: “Kama kweli Yanga wanataka kumrudisha Makambo, mimi sioni shida yoyote, kwa sababu ni mchezaji ambaye aliishi na kupendwa na mashabiki wa timu hiyo na Dar es Salaam aliishi kama nyumbani, sawa kama wanamtaka, lakini lazima wamlipe mshahara mzuri kama anaolipwa Horoya,” alisema Zahera.
Makambo aliichezea Yanga kwa msimu mmoja, 2018/19 na kufanikiwa kuifungia mabao 17 katika ligi kuu, kisha akatimkia Horoya ambako bado ana mkataba wa miaka miwili.