KAMPUNI ya GSM ipo katika hatua za mwisho za kuingia makubaliano na moja ya klabu za Hispania iliyopo kwenye viwango vya nne bora katika uendeshaji wa klabu ikiwemo kufanya ‘scouting’ ya wachezaji kabla ya kuwasajili.Wakati ikiahidi hayo yote, tayari GSM imeweka kitita cha Sh Bil 1.5 Yanga kwa ajili ya kufanikisha usajili wa wachezaji wapya kwenye msimu ujao.
Kampuni hiyo tayari imejitosa rasmi katika kusimamia mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo ikiwa tayari imepanga kumleta mtaalam kutoka Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) atakayesimamia mchakato mzima.Akizungumza na gazeti la Championi JUmamosi,Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said alisema kuwa mchakato mzima tayari umekamilika wa kusaini mkataba na klabu hiyo kubwa ya Hispania iliyopo kwenye ‘top 4’ La Liga.
Hersi alisema kuwa makubaliano watakayoingia na klabu hiyo ni kushirikiana katika idara zote za uendeshaji wa klabu ambazo ni program za mazoezi, vifaa vitakavyotumika mazoezini, ufundishaji na ‘scouting’ ya wachezaji ambao wao wanawataka kwa ajili ya kuwasajili.Aliongeza kuwa ni kuona Yanga inafikia levo za kimataifa na inapiga hatua kimaendeleo kama zilivyo klabu za Orlando Pirates, Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs zote za Afrika Kusini.
“Tupo Yanga kwa ajili ya kuipa maendeleo, tuna malengo makubwa, na kikubwa kuona tunafikia levo za kimataifa na siyo kuishia kitaifa na ndiyo sababu ya kuwepo katika hatua za mwisho za kukamilisha kuingia makubaliano ya kimkataba na moja ya klabu kubwa ya La Liga.
“Mkataba huo tutakaoingia ni wa jinsi ya uendeshwaji wa klabu, tunataka kuona Yanga inajiendesha kisasa na siyo kizamani na ndiyo sababu ya sisi GSM kusimamia mfumo huo mpya wa uendeshaji wa klabu.“Hivyo, tupo tayari kugharamia kiasi chochote cha fedha ili kufanikisha hilo, kamati husika zitakazosimamia mfumo huo tayari zimechaguliwa na Mwenyekiti Msolla (Mshindo), hivyo wakati wowote utaanza,” alisema Hersi.
Stori na Wilbert Molandi | Championi Jumamosi