Home Uncategorized KUHUSU YANGA….CHAMA AMTAJA NIYONZIMA..!!

KUHUSU YANGA….CHAMA AMTAJA NIYONZIMA..!!

HIVI karibuni mashabiki wa Simba walikuwa na presha baada ya kuzagaa kwa taarifa kuwa Yanga wako katika mchakato wa kumnasa kiungo wao, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ a.k.a Triple C.

Lakini mchezaji mwenyewe akiwa kwao Zambia, aliamua kufunguka juzi Ijumaa mchana kwenye akaunti yake ya Instagram alipokuwa ‘live’ akijibu maswali ya mashabiki wa soka Afrika.

Alianza kwa kusisitiza kuwa ana furaha kuendelea kukipiga Simba, sababu iliyomfanya kujiunga na miamba hiyo ya soka la Tanzania na mengine kibao. “Hapana siwezi kwenda Yanga kwa sababu bado nina mkataba na Simba, nina furaha hapa na kwa sasa nipo nyumbani (Zambia), nitarudi muda sio mrefu bado nina kazi ya kufanya, msimu haujamalizika,” alisema staa huyo ambaye timu yake inaongoza kwa pointi 71, ikifuatiwa na Azam (54), Yanga ikiwa nafasi ya tatu na alama zao 51.

KWANINI SIMBA?

Chama anasema sababu iliyomfanya kujiunga na Simba mwaka 2018 akitoka kuichezea Lusaka Dynamos FC ya nchini kwao ni malengo ya klabu hiyo. “Malengo ya Simba ni kuwa miongoni mwa klabu kubwa barani Afrika. Hilo lilinisukuma na sio kitu kingine,wanafanya mambo kwa malengo,” anasema Chama mwenye miaka 28.

KUHUSU NIDHAMU

Chama ni miongoni mwa nyota wa Simba wanaotajwa kuwa na nidhamu mbovu, hakulifumbia macho akisema kila mtu ana uhuru wa kusema lolote analojisikia.
“Sijui hilo lina ukweli kiasi gani, lakini watu muda wote wanaweza kusema wanachojisikia kuhusu yeyote. Siwezi kupingana na maneno yao kwani nami pia ni binadamu.” Ishu ya kushindwa kudhibiti nidhamu ya wachezaji ndani ya Simba ilielezwa ni miongoni mwa sababu zilizomfanya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems kuondolewa.

YANGA ATAJWA NIYONZIMA

Miongoni mwa nyota wa Yanga ambao Chama anakubali uwezo wao ni pamoja na Haruna Niyonzima ‘Fabregas’.
“Kwa Yanga namkubali Niyonzima,” anasema Chama bila kutafuna maneno. Niyonzima na Chama walicheza pamoja katika kikosi cha Simba, aina yao ya soka imekuwa ikiendana.

HATAISAHAU SEVILLA

Chama anasema hawezi kusahau mchezo wa kirafiki aliocheza dhidi ya Sevilla ya Hispania ambao Simba walikumbana na kipigo cha mabao 5-4. “Ulikuwa mchezo bora kwangu ushindani ulikuwa wa kiwango cha juu mno.” Katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa Mei, mwaka jana, John Bocco, nahodha wa Simba aliitanguliza kwa bao la mapema la dakika nane kabla ya Meddie Kagere kuongeza la pili dakika ya 15.
Sergio Escudero alifungua kalamu ya mabao kwa Sevilla kwa bao la dakika ya 24 kabla ya Bocco tena kuipeleka Simba mapumziko na mabao 3-1.
Kipindi cha pili, Simba iliendelea kushambulia kwa kasi, ikiacha Sevilla ikimiliki mpira kabla ya kumsahau mkongwe Nolito kupunguza uongozi wa Simba kwa bao la dakika ya 49. Kuingia kwa bao hilo kuliongeza hamasa ya wachezaji wa Sevilla walioongozwa na Wissam ben Yeder, Ever Banega, Aleix Vidal, Jesus Navas na Sergio Escudero. Licha ya Chama kuongeza bao la nne kwa Simba, mabao matatu ya lalasalama ya Promes, Munir na Nolito yaliwafanya Simba kupoteza mchezo huo.

AMTAJA GAUCHO

Kati ya wachezaji anaowakubali katika kikosi cha Simba Queens kinachoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ni Mwanahamisi Omary maarufu kama Gaucho. “Ni mchezaji mwenye kipaji. Anajua.”

MSOSI YUMO, familia

Chama humwaambii kitu mbele ya chapati, ugali na samaki, ndizi pamoja na firigisi. “Hivyo vyakula nimekuwa nikipenda kula muda wote sijawahi kuvichoka.”
Kuhusu familia, Chama anasema ana mke aitwaye Annalisa Mercy Chama na bahati nzuri wamepata watoto watatu na hana mpango wa kuongeza mwingine. “Nina furaha na familia yangu, sina mpango wa kuwa na mke mwingine.”

MUZIKI, NAFASI ANAYOPENDA

Kama ilivyo kwa wachezaji wengine Chama ni mfuasi wa muziki na kati ya wasanii wa Tanzania ambao anapenda kusikiliza kazi zao ni Diamond na Harmonize. “Napenda kusikiliza muziki ila wasanii wengine majina yao siyakumbuki ila Diamond na Harmonize napenda nyimbo zao, mfano Baba Lao.”
Mbali na kuona muda mwingine akicheza kama winga wa kulia au kiungo wa kati kama namba nane, Chama anasema kati ya maeneo ambayo amekuwa akiyafurahia kucheza ni pamoja na winga wa kushoto na nyuma ya mshambuliaji.
SOMA NA HII  SABABU YA SENZO KUBWAGA MANYANGA SIMBA NA KUIBUKIA YANGA IPO HIVI