SHUGHULI ambayo alikuwa akiipata Mzimbabwe Tafadwa Kutinyu kutoka kwa mabeki Kelvin Yondani wa Yanga na Erasto Nyoni wa Simba ilikuwa ikimfanya kutumia dawa za kupoza maumivu staa huyo wa zamani wa Singida United na Azam.
Kutinyu ambaye kwasasa yupo Guinea katika klabu ya Horoya alisema Yondani na Erasto ni mabeki ambao walikuwa wakimsumbua huku muda mwingine wakimwachia majeraha.
Alisema mbali na uwezo wao wa kukaba, mabeki hao wa Taifa Stars hasa Yondani ni hodari wa kucheza mchezo ambao sio wa kiungwana.
“Nimecheza dhidi ya mabeki wengi wazuri Tanzania lakini Yondani na Erasto walikuwa kiboko, ni wazoefu na wajanja,kuwatoka inatakiwa utumie akili ya ziada.
“Nimekumbuka mengi ya Tanzania. Vile ambavyo nilikuwa nikiishi na wachezaji wenzangu kama familia moja, utani ulitufanya tushibane, nilifurahia sana soka nikiwa na Hans van der pluijm,” alisema.
Kutinyu alijiunga na Horoya akiwa na mastaa wengine, Enock Atta Agyei aliyekuwa Azam na Heritier Makambo ambaye alitesa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Yanga.
Mzimbabwe huyo, alisema amekuwa na ushirikiano mzuri na wachezaji wenzake hao ambao alicheza nao soka nchini, “Tumekuwa tukikabiliana na changamoto mpya za soka huku pamoja, tunatiana moyo.”