Home Uncategorized KUHUSU KUPAMBANA NA CORONA WACHEZAJI FANYENI HIVI

KUHUSU KUPAMBANA NA CORONA WACHEZAJI FANYENI HIVI


MANAHODHA wa Bongo wakati wa kuzinduka na kuendeleza ile vita ya kupambana na adui Corona kwa vitendo ni sasa kwani hakuna muda mwingine ambao tutapata wa kuanza kupambana kwa vitendo.
Hali sio shwari kwenye dunia kwani mtikisiko ambao umepita ni mkubwa hivyo ni lazima  wenye busara ambao ni viongozi watakakoanza kuutuliza mtikisiko wa namna hii wawepo.
Miongoni mwa wanaoweza kuwa mstari wa mbele katika hili ni manahodha wa timu zote Bongo kuanzia zile zinazoshiriki Ligi Kuu Bara mpaka zile za hatua ya ngazi ya vijiji bado ni timu.
Ninatambua kwamba kwenye mitaa pia kuna timu ambazo zina manahodha wao zile ambazo zinapiga mpira wetu wa kitaa tunaziita chandimu bado ni timu pia zinawatoa wachezaji wengi tu.
Kuanzia makapteni wa chandimu ni muda wa kuungana na kuwa na nguvu moja katika mapambano dhidi ya Corona kwani kwa namna moja ama nyingine katika michezo yote pande zote zinatugusa pia.
Enzi zile wakati tunarukaruka kwenye madarasa yaliyojengwa na mababu zetu achana na madarasa ya sasa ambayo mbele kuna ubao mweusi na mwalimu anashika chaki kisha anaandika nawe unagandamizia.
Hapa nazungumzia madarasa yale yaliyokuwa chini ya mwembe, kwa wapenda shule walikuwa wanaichukia mvua kwa kuwa ikinyesha hapo ndio mapumziko yanaanzia.
Sasa wakati ule tulikuwa tunafundishwa kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu ninaaona kwamba iwapo manahodha wote wataungana katika hili itaongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya Corona.
Hebu pata picha namna ambavyo John Bocco wa Simba alivyo na uwezo katika kukiongoza kikosi cha Simba kwa mfano akisema kuwa anaanzisha mfuko ambao wachezaji wote Bongo watatupia hata buku tano hivi kwa ajili ya Corona unadhani nini kitatokea.
Kisha sapoti kubwa ataipokea kutoka kwa mtu wa watu Pappy Tshishimbi nahodha wa Yanga na sapoti pia kwa Relliats Lusajo yule wa Namungo mambo yatakwenda kwa kasi.
Achana na hao yupo mkongwe wao ambaye ana busara pia huyu hapa Juma Kaseja anayekipiga ndani ya KMC unadhani akitoa neno katika hili kwamba kwa yoyote yule ambaye ni mchezaji ajitoe kwa ajili ya kupambana na Virusi vya Corona.
Ngoma itakuwa bado haijapoa kuna Jaccob Massawe yeye anawakilisha Gwambina unadhani atagomea wazo kama hili wakati huu wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona?
Wengi huwa tunawaskia kwenye vyombo vya habari kwamba mnawatazama wale wanaokipiga nje akina Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Mohamed Salah  kwa namna wanavyofanya basi na yale ambayo wanayafanya tuyaige pia.
Tunaona kwamba wenzetu wanaoshiriki Ligi Kuu England kupitia kwa manahodha wameungana na wanaendeleza sapoti kwa ajili ya kupambana na Corona.
Hakuna baya kuiga katika hili ni jambo jema na linapendeza pia hivyo italeta maana ikiwa kutakuwa na mfuko Bongo unaowahusu wachezaji pekee wakiungana na Serikali katika kupambana na Virusi vya Corona.
Tunaona kwamba Serikali imekuwa bega kwa bega kaika masuala yanayohusu michezo na inatoa sapoti kubwa katika kila hatua basi na katika hili tuungane wanafamilia ya michezo ili kushinda kwa pamoja.
Haina maana kwamba wanafamilia ya michezo tupo nyuma  hapana ila kuna mambo ambayo kwa sasa yanatakiwa yafanyike ili kesho itakapofika kila mmoja atambue kwamba alihusika kwa namna gani kupambana na vita hii.
Ni ngumu kuamini kwamba kwa sasa hakuna ambaye hana maumivu katika hili janga ila ni muhimu kutambua kwamba kazi yetu moja kubwa kwa sasa ni kuendelea kupambana mpaka hatua ya mwisho.
Kuwa mabalozi nyumbani na kwa familia pekee bado ni deni kwetu kwa ajili ya wengine na wale ambao wanafuatilia kwa kuonyesha kwamba tupo pamoja na tunajali.
Hakuna mkataba wa kunyoosha mikono wakati huu mapambano lazima yaendelee ili kuona namna gani tutaibuka vifua mbele.
Manahodha wasaidizi nao pia nina amini hamtawaangusha viongozi wenu katika hili la kupambana na Virusi vya Corona.
Mzee wa kumwaga maji Juma Abdul wa Yanga, Mohamed Hussein wa Simba ni wakati wa kuendelea yale mavitu ya uwanjani kwa jamii na kwa vitendo.
Italeta picha nzuri kwamba wakati ule vita inakwishwa nasi pia tunakuwa ni sehemu ya ushindi wa vita hii ambayyo imefanya mambo mengi kusimama.
Kusimama kwa michezo kunatukosesha ule uhondo ambao tulikuwa tumeuzoea hasa kwenda kuona namna ushindani ulivyo na mpaka mshindi anapatikana.
Kwa sasa mambo yamekuwa yakienda kwa kusuasua kutokana na shughuli nyingi kusimama kwani licha ya kwamba bado watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kiasi fulani kuna anguko kwenye suala la ajira za watu binafsi.
Ndugu zetu waliokuwa wakionyesha mechi kwenye vibanda umiza kwa sasa hawana chaguo la kufanya zaidi ya kubadili mipango upya.
Yote kwa yote jukumu ni letu kupambana kwa vitendo mpaka pale tutakaposhinda na kuwa pamoja katika maisha ya kawaida.
SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU