KIUNGO wa Simba, Luis Miquissone, ameibuka na kusema kuwa anatamani kuona janga la ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na Virusi vya Corona, lipotee ili waweze kurejea uwanjani kupigania ubingwa wao wa msimu huu.
Luis ambaye kwa sasa yupo kwao Msumbiji, ametoa kauli hiyo ikiwa Simba inaongoza ligi kwa pointi 71 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 54, wakati Yanga wakiwa kwenye nafasi ya tatu na pointi 51 huku Namungo nafasi ya nne kwa pointi 50 tangu ligi ilipotangazwa kusimama kutokana na Virusi vya Corona vinavyoendelea kuishambulia dunia.
Luis amesema kuwa kwa sasa anatamani kuona ugonjwa huo unapotea ili waweze kurejea uwanjani kupigania ubingwa wao katika michezo iliyobakia kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
“Nimekuwa nikikumbuka kucheza mpira lakini haiwezekani kwa sababu ya Corona, nafanya mazoezi kutokea nyumbani na kuendelea kujilinda katika kipindi hiki kigumu kwa kuwa ni tatizo ambalo dunia nzima bado haijaweza kulipatia ufumbuzi kitu ambacho kimepelekea kuharibu kila kitu.
“Unajua sisi tunaongoza ligi na matarajio ni kuweza kuchukua ubingwa na ndiyo malengo ya timu lakini Corona imezuia kuendelea na ligi lakini natamani kuona imeisha ili kuweza kurejea uwanjani na kuona tunamalizia mechi zilizobaki kwa ushindi ili tuchukue ubingwa,” amesema Luis.