Home Uncategorized MPANGO WA KUREJESHA LIGI,TFF KUNA UMUHIMU WA KUWA NA MKAKATI WA KIPEKEE...

MPANGO WA KUREJESHA LIGI,TFF KUNA UMUHIMU WA KUWA NA MKAKATI WA KIPEKEE KULINDA AFYA ZA WACHEZAJI


HATMA ya Ligi Kuu Bara bado haijulikani itakuaje kwa sasa kutokana na mambo mengi kusimama na kushindwa kuendelea kufanyika kama ilivyokuwa awali.
Sababu kubwa ya yote kwenda kwa mtindo huo ni kutokana na janga la Virusi vya Corona ambalo linaitaikisa dunia nzima kwa sasa.
Majirani zetu Kenya wao wamemaliza kabisa utata kwa kumaliza ligi yao kwa kumpa ubingwa kinara wa ligi ya Kenya ambaye ni Gor Mahia.
Katika hili ninawapa pongezi kwani wamefanya maamuzi mazuri ambayo ni kwa ajili ya faida ya kizazi cha Kenya kijacho na kile cha sasa.
Kenya wameona busara kumpa ubingwa anayeongoza ligi huku mpango wa timu ambazo zitapanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza ukiwa ni kucheza play off kwa timu shiriki.
Hii inawezekana kwa kuwa mechi za play off sio zaidi ya 10 na zinaweza kuchezwa kwa muda ambao dunia itakuwa imeanza kupata nafuu kutoka kwenye janga la Corona.
Ni muhimu pia kutazama maamuzi mazuri kwa ajili ya taifa na sio lazima kila mmoja afurahie kile unachokifanya ukiwa kiongozi unaaminiwa na unapaswa utoe maamuzi ambayo yana busara na hekima kwa wale unaowaongoza.
Ni muda wa Shirikisho la Soka Tanzania kutazama upya ni namna gani wanaweza kumaliza nao ligi kwani siku hazigandi zinakwenda kwa kasi sana.
Kila mmoja anaongea jambo lake na kuzungumza yale anayotambua ila mwisho wa siku wenye maamuzi kuhusu hatma ya ligi ni mamlaka yenyewe ambayo ni TFF.
Rais wa TFF, Wallace Karia katika hili unahitaji utumie busara zaidi na kufanya vikao na jopo lako la washauri ili kujua hatma ya ligi itakuajekuaje, kukaa kimya sio dawa ya kumaliza tatizo.
Tunaona kwamba kule Ulaya wale wa Ligi Kuu England wameweka mkakati wao kwamba kabla ya ligi kurejea wachezaji watakaa karantini kwa muda wa wiki sita ili kuwatazama hali zao zipoje.
Pia mechi zao zitachezwa bila ya kuwa na mashabiki ili kuzuia maambukizi zaidi kwani hili janga ni balaa ni lazima kujilinda katika kila namna.
Tayari wenzetu wameanza kuonyesha hata zile dalili kwamba ligi inaweza kurudi na kuna maandalizi ambayo yanafanyika je kwa hapa Bongo nini kinafanyika?
Kuanza kwa ligi katika nyakati hizi ngumu kunahitaji moyo mgumu na ili kuondoa hizo hofu ni lazima kuwe na maandalizi makini ambayo yatafanya kila mmoja awe salama.
Utajiri namba moja ni afya hivyo katika hilo TFF mna kazi ya kutazama namna gani mtalinda afya za wachezaji pamoja na mashabiki.
Pia ni muhimu kuanza maandalizi kwa sasa ikiwa kuna uwezekano wa ligi kurejea ili kuwaandaa wachezaji pamoja na timu katika utayari kwani wengi wao bado hawaelewi wafanye nini kwa sasa..
Mwisho wa yote ni kwamba lazima tutambue kuwa yote tunayofanya kila mmoja asisahau kuchukua tahadhari ili awe salama na kufuata kanuni za afya ni jambo la msingi.
 Licha ya kwamba Serikali imesema inafikiria kurejesha ligi bado kuna umuhimu wa TFF kuangalia namna bora ambayo inaweza kufanya ligi ikachezwa ili kuepusha zaidi zile safari ka timu kwenda mkoa mwingine. 
Kila mmoja anapenda kuona mpira hata mimi ninapenda lakini usalama wa wale wanaocheza i muhimu na mikakati mizuri inahitajika.
SOMA NA HII  LIPULI:NJOONI SAMORA MPATE BURUDANI