FRANCIS Kahata, kiungo mshambuliaji wa Simba amesema kuwa ana matumaini makubwa ya Klabu yake kuchukua ubingwa kutokana na nafasi ambayo wapo kwa sasa.
Simba ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 28 kibindoni ina pointi 71.
Tangu Machi 17 hakukuwa na shughuli za michezo baada ya kusimamishwa kutokana na janga la Virusi vya Corona. Serikali imeruhusu masuala ya michezo kuanza leo Juni Mosi huku ratiba ikieleza kuwa mechi za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili zitaanza Juni 13.
Kahata amesema:”Kuna ushindani mkubwa ambao upo lakini kwa kuwa tulikuwa sehemu nzuri imani ya kufanya vema ipo na nafasi ya kutwaa ubingwa pia.
“Wachezaji tulikuwa tunafanya mazoezi wakati wa mapumziko yalisyosababishwa na Corona,tumerejea tutaendelea pale ambapo tuliishia,” amesema.
Kahata ni miongoni mwa nyota wa Simba ambao walisepa Bongo na kurejea kwao Kenya, alirejea Mei 31 na kuungana na wachezaji wenzake ambao waliripoti kambini Mei 27.