JUNI 13, burudani iliyokosekana kwa muda mrefu ya soka ilirejea rasmi baada ya Serikali kuruhusu masuala ya michezo kuendelea kama kawaida huku tahadhari zikiendelea kuchukuliwa.
Ikumbukwe kuwa masuala ya mijumuiko isiyo ya lazima ilisimamishwa Machi 17 na Serikali kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vinaivuruga dunia.
Wakati ligi ikisimamishwa kuna nyota wa timu mbalimbali wao walikuwa wametupia bao mojamoja hivyo wana kazi kuendelea kuongeza idadi ya mabao, hapa tunakuletea kosi kamili namna hii.
Dida
Deogratius Munish, ‘Dida’ Februari 11, alitupia bao lake mbele ya Mbeya City wakati Lipuli ikipoteza kwa kufungwa mabao 2-1, Uwanja wa Sokoine, alifunga kwa penalti.
Ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20, Dida anashikilia rekodi ya kuwa kipa aliyefunga. Kwenye mchezo huo mabao yote matatu yalifungwa kwa mikwaju ya penalti kwa Mbeya City, Peter Mapunda alijaza nyavuni bao moja pia.
Tairone Santos
Tairone Santos, Novemba 23, Uwanja wa Uhuru ilikuwa mbele ya Ruvu Shooting yenye sera ya kupapasa iliyoasisiwa na Masau Bwire.
Ngoma ilikamilika kwa Simba kusepa na pointi tatu na ilishinda kwa mabao 3-0, beki huyo raia wa Brazil alishangilia kwa nguvu zote akifurahia kufunga bao lake la kwanza kwenye ardhi ya Bongo.
Nicolas Wadada
Nicolas Wadada, Novemba 8, mwaka jana alifunga bao moja dhidi ya Biashara United. Azam FC ikisepa na pointi tatu mazima mbele ya Biashara United, Wadada aliwatungua bao moja wapinzani wao.
Kinara huyo wa kutengeneza pasi raia wa Uganda akiwa amejiwekea kibindoni pasi saba alifunga bao lake la kwanza kwa pasi ya kinara wa kutupia ndani ya kikosi hicho Obrey Chirwa mwenye mabao nane.
Yakub Mohamed
Beki huyu raia wa Ghana ni kisiki ndani ya kikosi cha Azam kwani amekuwa ni mhimili mkubwa jambo ambalo limewavutia Simba ambao wanahaha kupata saini yake.
Bao lake alifunga kwenye mchezo dhidi ya Mbao kwa kuachia shuti kali akimalizia pasi ya Donald Ngoma ambaye ni mshambuliaji.
Erasto Nyoni
Mbele ya Azam FC, Uwanja wa Taifa, Nyoni aliwatungua waajiri wake wa zamani Azam FC, wkati timu yake ikishinda kwa mabao 3-2. hiyo ilikuwa Machi 4, mwaka huu.
Nyoni ni kiraka alirekebisha makosa yake kwa kusawazisha bao walilofungwa dakika ya nne na Never Tigere aliyemtungua Aishi Manula.
Abdulaziz Makame
Kiungo huyo aliwatungua Coastal Union, Uwanja wa Uhuru, Oktoba 6 alipachika bao hilo kwa kichwa akimalizia pasi ya kichwa cha beki mwenzake Ally Ally na kuipa ushindi timu yake ambayo ilizibeba pointi zote tatu.
Yikpe Gnamien
Mshambuliaji huyu wa Yanga aliwafunga Singida United, Uwanja wa Namfua kwa kichwa ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza baada ya kutua ndani ya Yanga na kusaini kandarasi ya miaka miwili akitokea Klabu ya Gor Mahia ya Kenya
Ilikuwa ni Januari 22, Yanga ilishinda mabao 3-1.
Salim Aiyee
Straika huyu wa KMC alifunga bao lake pekee kwa msimu huu mbele ya Yanga, Machi 12 katika Uwanja wa Uhuru na kuipa timu yake pointi tatu na kuifanya timu hiyo kuwa moja ya waliobeba pointi tatu za Yanga.
Ibrahim Ajibu
Uwanja wa Taifa Ajibu aliwaua Polisi Tanzania dakika za mwishoni kabisa na lilikuwa ni bao lake la kwanza ndani ya msimu wa 2019/20 baada ya kujiunga ndani ya kikosi hicho akitokea Klabu ya Yanga.
Simba ilishinda mabao 2-1, ilikuwa Februari 5 alifunga bao hilo kwa pasi ya upendo kutoka kwa kiungo mwenzake Francis Kahata.
Mudathir Yahya
Mbele ya Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru, kiungo huyu mzawa alifunga bao lake la kwanza msimu huu akimalizia pasi ya Nicolas Wadada.
Mchezo huo uliokuwa ni wa kukata na shoka Azam ilishinda kwa bao moja ambalo Yahya alijikunjua akiwa nje ya 18 na kumuacha mlinda mlango wa Polisi Tanzania, Mohammed Yusuph akawa hana la kufanya ilikuwa ni Februari 11.
Haruna Niyonzima
Niyonzima alifunga bao lake mbele ya Singida United Uwanja wa Namfua, Januari 22 kwa pasi ya kiungo Bernard Morrison.
Dakika 90 zilikamilika kwa Yanga kuwaachia joto la jiwe ‘walima alizeti’ kwa ushindi wa mabao 3-1.