Na Saleh Ally
MWANADAMU huwa anafanya makosa na kama ni muungwana huwa kinachofuatia ni kujuta, sote tunalijua hili na lazima tumewahi kulipitia bila ya kujali ukubwa au udogo wake.
Niseme ninaungana na kila mpenda michezo na hasa soka ambaye amekerwa na kitendo cha beki wa Yanga, Lamine Moro raia wa Ghana kumkanyaga mgongoni Mwinyi Kazimoto baada ya kutokea tafrani dakika za mwisho za mchezo huo ulioisha kwa sare.
Kama utaona kuna mtu anakataa kuwa Moro asipewe adhabu, kuna mambo mawili yatakuwa yamemtawala. Moja ni ushabiki uliopindukia, pili ni kukosa uungwana wa kuwajali watu wengine kama wanadamu.
Sitaki kuingiza utaifa katika hili na kusema Kazimoto ni Mtanzania mwenzangu lakini nataka tulijadili kama jambo lisilo sahihi hata kama lingekuwa limefanywa na Mtanzania mwenzetu.
Tunataka kuendelea kutimiza Fair Play katika soka, tulikubali kuwa soka ina ushindani lakini soka ni uungwana. Hivyo si sahihi kwa yoyote yule anayewashambulia wenzake.
Kitendo alichokifanya Lamine si cha kiungwana, Kazimoto hakuwa mtu hatari kwake, hakuwa akimshambulia na hakuwa amefanya jambo lolote baya dhidi yake. Alisukumana na wachezaji wa Yanga, nao wakamsukuma, jambo ambalo katika soka ni la kawaida sana.
Nimeona baadhi ya mashabiki katika mjadala wao wanataka kuhalalisha upuuzi wa Lamine, eti hata mchezaji kama Zinedine Zidane aliwahi kufanya hivyo kwa kumpiga kichwa Marco Materazzi wa Italia. Huu ni upuuzi wa kiwango cha lami.
Lamine hakuwa ametukanana au kukashifiana na Kazimoto, hawakuwa wamebishana lolote na ukiangalia hana hata sababu nusu ya kulazimika kufanya vile. Bora angetumia mikono kumsukuma kuliko kutaka kumvunja mgongo kwa kuhatarisha maisha yake.
Kiukweli, ni jambo linalokera sana na linaweza kuwa linakera zaidi kama utafikiria mchezaji kama Lamine ni mgeni na kawaida tunakuwa tunatarajia kuona mambo mengi mazuri ya kujifunza kutoka kwa kwake kuliko upuuzi kama huo ambao unaonyesha kuna walakini mkubwa.
Kwa namna nimezoea kumuona Lamine, anaonekana ni mtu mwenye busara na ambaye anaweza kuwa kiongozi uwanjani na si mjinga kama ilivyotokea.
Niko upande wake kiasi fulani, kwamba pamoja na upuuzi mkubwa alioufanya lakini pia ndani ya tatizo hilo ametoa funzo ambalo si kawaida yetu katika mpira wa Kitanzania. Ameomba msamaha kwa maandishi na baadaye kwa video yaani maneno, huu ni uungwana.
Amemuomba msamaha Kazimoto, Watanzania wote na TFF kutokana na alichokifanya na akasisitiza kwamba atampigia simu Kazimoto na kumuomba radhi moja kwa moja kwa kuwa anakijutia kitendo chake.
Kawaida unapofanya kazi ili uwe muungwana, kuna mambo matatu yatatokea. Kwanza kulikubali kosa, pili kulijutia, tatu kuomba msamaha. Lamine hadi anafikia kuomba msamaha, hayo mawili ya nyuma lazima ameyapitia kufikia hilo la tatu.
Ndiyo maana ninaamini hivi, ana kichwa kizuri kinaweza kutafakari mambo ingawa hakufanya hivyo kabla lakini utukutu wa miguu yake, ulimzidi nguvu na kuchukua uamuzi mbaya ambao leo unakiponza kichwa chake.
Kama amefikia kufanya hivyo, kapita hatua zote tatu maana yake tunaamini hatarudia na atakuwa amejifunza kwa upuuzi alioufanya.
Pamoja na hivyo, bado ningesema anastahili adhabu ili liwe funzo. Sijajua kama inaweza kupungua kutokana na hatua alizozichukua za kiungwana au la lakini itakuwa vizuri aadhibiwe kwa kuwa wengine pia watajifunza ili isije ikawa watu wengine waharibu kwa makusudi halafu waamini kumba msamaha itakuwa ndiyo kinga.
Baada ya hapo, uongozi wa Yanga nao wapokee pongezi zangu. Wametuonyesha mchezo wa soka unaweza kubadilishwa na watu wenye mawazo chanya hasa baada ya kuchukua hatua mara moja kuomba msamaha kutokana na kitendo cha mchezaji wao aliyefanya kosa katika hadhira kubwa yenye watu wa Kariba, umri na heshima tofauti.
Pamoja na hivyo, wamemuadhibu na hili liwe fundisho kwa viongozi wa klabu nyingine kuhusiana na suala la kusisitiza nidhamu na upendo hata kwa wapinzani. Soka si vita.
Tatizo la beki Lamine Moro kumkanya kiungo mkongwe wa JKT Tanzania, wine Kazimoto limefunika mambo mengi sana yaliyotokea katika mchezo kati ya Yanga dhidi ya wanajeshi hao, juzi.