MABINGWA watetezi wa Kombe la Ligi Kuu Bara, Simba jana wameishushia kichapo cha mabao 2-0 Mbeya City kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Sokoine.
Simba iliyo chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroec ilianza kutupia bao la kwanza dakika ya tano kupitia kwa nahodha wao John Bocco lililoipeleka Simba mapumziko wakiwa kifua mbele kwa bao hilo.
Juhudi za Mbeya City, inayonolewa na Amri Said kutafuta matokeo kupitia kwa mshambuliaji wao namba moja Peter Mapunda mwenye mabao tisa ziligonga mwamba kwa kuishia mikononi mwa mlinda mlango wa Simba Aishi Manula aliyekuwa akilindwa na Pascal Wawa pamoja na Shomari Kapombe.
Bao la pili lilipachikwa na Bocco dakika ya 54 baada ya dakika tisa kupita kwenye kipindi cha pili cha mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 78 baada ya kucheza mechi 31 huku wakifunga jumla ya mabao 69 na kujikita kileleni.
Mbeya City mambo bado magumu kwani ipo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 31 ina kibarua kizito cha kutetea nafasi ya kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kubakiza mechi moja tu ili kutwangazwa kuwa mabingwa kwani wakishinda watafikisha pointi 81 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote kwa sasa.
Kupoteza kwa Azam FC kwa kufungwa bao 1-0 mbele ya Kagera Sugar kumewafanya wabakie nafasi ya pili wakiwa na pointi 58 huku Yanga iliyolazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na Namungo ikibaki nafasi ya tatu na pointi zake 57. Timu zote zimebakiwa na mechi saba ambazo ni sawa na pointi 21.
Ambapo Azam akishinda zote atafikisha jumla ya pointi 79 na Yanga ikishinda zote itafikisha jumla ya pointi 78 ambazo zitakuwa zimeshapitwa na Simba.
Vita kubwa kwa sasa ni kwenye nafasi ya pili ambapo Yanga na Azam FC zitakuwa zinapambania ikiwa Simba itaweza kushinda mbele ya Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Juni 28.