Home Uncategorized KUHUSU KUTUA YANGA..KOTEI AMEFUNGUKA HAYA..!!

KUHUSU KUTUA YANGA..KOTEI AMEFUNGUKA HAYA..!!

UJUMBE wa kiungo wa zamani wa Simba, James Kotei (26) alioutuma leo kwenye ukurasa wake wa Instagram, umeonyesha ishara ya wazi kuwa anaelekea kujiunga na watani wao wa jadi Yanga, katika dirisha lijalo la usajili.

Kotei ambaye hivi karibuni alivunja mkataba na timu yake ya Slavia Mozyr inayoshiriki Ligi Kuu ya Belarus, kupitia ujumbe huo ametoa kauli inayoonekana ya kuwaandaa kisaikolojia mashabiki wa Simba aliyoicheza kwa mafanikio kuwa anaelekea kujiunga upande wa pili.

Katika ujumbe huo, Kotei ameweka picha inayomuonesha akiwa yeye pamoja na beki Erasto Nyoni na mshambuliaji Emmanuel Okwi, wakishangilia bao la Simba pindi alipokuwa akiichezea timu hiyo na kuweka ujumbe wa kuonyesha kuwa anaelekea kuwa mpinzani wao.

“Rafiki wa jana ni adui wako wa kesho. Angalia vyema urafiki wako. Nikiwa na beki wa kati mwenye akili, Erasto Nyoni na mshambuliaji fundi, Emmanuel Okwi. Muwe na wiki njema familia,” aliandika Kotei.

Yanga imekuwa ikimuwinda Kotei kwa muda mrefu tangu alipoachana na Simba mara baada ya msimu uliopita na inatajwa kuwa mazungumzo baina yao na kiungo huyo yapo katika hatua nzuri na kinachosubiriwa ni Kotei kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.

Hilo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na kitendo cha hivi karibuni cha kiungo huyo, kuvunja mkataba wake na timu ya Slavia Mozyr aliyokuwa akiichezea, ambao unatajwa kuwa ndio ulikuwa kikwazo kwake kumalizana na Yanga.

Kotei alitamba vilivyo pindi alipoitumikia Simba kuanzia mwaka 2016 akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili, ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam mara moja lakini pia kuisaidia kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019.

Hata hivyo baada ya kuondoka Simba, mambo yalianza kumuendea kombo kwani hakupata nafasi katika kikosi cha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo alijiunga nacho na kisha mwezi Disemba, 2019 akavunjiwa mkataba.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMAMOSI