Home Uncategorized MOLINGA, KASEKE WAKIWASHA TAIFA WAKIIMALIZA KAGERA SUGAR MABAO 2-1, AWESU MUACHE KABISA

MOLINGA, KASEKE WAKIWASHA TAIFA WAKIIMALIZA KAGERA SUGAR MABAO 2-1, AWESU MUACHE KABISA


YANGA leo imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho uliochezwa Uwanja wa Taifa.

Kagera Sugar inayonolewa na Mecky Maxime itajilaumu yenyewe kipindi cha kwanza kwa kushindwa kutulia na kutumia nafasi ambazo walizitengeneza kwani walikuwa kwenye ubora upande wa kiungo wakiwapoteza mazima wachezaji wa Yanga.

Bao la Kagera Sugar lilipachikwa kiufundi na nyota wao Awesu Awesu mwenye rasta kichwani ambaye alifunga akiwe nye kidogo ya 18 akimalizia pasi ya kisigino ya Yusuph Mhilu dakika ya 19.

Yanga walikwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0 ambapo kipindi cha pili walifanya mabadiliko kwa kumtoa Ditram Nchimbi na nafasi yake ikachukuliwa na Mrisho Ngassa mwamba wa ziwa Victoria mzee wa enjoi soka.

Dakika ya 52 Molinga alifunga bao la kuweka usawa akimalizia pasi ya kichwa ya Ngassa naye akifunga bao la kichwa na kuwarudisha mchezoni Yanga.

Katika harakati za Kagera Sugar kutaka kufunga, Awesu alionekana amechezewa faulo na Metacha Mnata ndani ya 18 mwamuzi wa kati akamuonyesha kadi ya njano ya kwanza Awesu.

Yanga iliandika bao la ushindi dakika ya 76 kupitia kwa Deus Kaseke ambaye alifunga bao hilo kwa penalti baada ya mwamuzi kutafsiri kuwa alichezwa faulo Mrisho Ngassa ndani ya 18.

Awesu baadaye alionyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kile ambacho mwamuzi alitafsiri namna anavyojua ndani ya uwanja kwani tukio lilionyesha kuwa alichezewa faulo, alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje dakika ya 78. 

Kwa sasa Yanga inakula upepo ikisubiri mshindi wa mchezo wa kesho kati ya Simba ama Azam hatua ya nusu fainali.

SOMA NA HII  BUKAYO SAKA AONGEZA DILI REFU NDANI YA ARSENAL