SVEN Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa siri kubwa ya wachezaji wake kufanya vizuri kwenye mechi zao nyingi ni kutumia akili na utulivu mkubwa ndani ya uwanja.
Viungo wake wawili, Clatous Chama na Miraj Athuman,’Sheva’ wamekuwa na wakati mzuri kila wanapopata nafasi ya kuanza kucheza jambo ambalo linamfanya awe na uhakika wa kupata matokeo pindi wanapoanza.
Wawili hao wamehusika kwenye jumla ya mabao 19 kati ya 76 yaliyofungwa na Simba ambapo Chama amefunga mabao mawili na pasi 9 za mabao 2 huku Sheva akiwa amefunga mabao 7 na asisti moja.
Sven amesema kuwa :-“Kila mchezaji ndani ya timu ni muhimu na wote wana nafasi zao katika kuzitimiza, huwa ninashindwa kuwatumia wote kwa kuwa nina wachezaji wengi na kanuni haziruhusu hayo yatokee, ila ukimzungumzia Chama, Miraj wanatumia akili na utulivu mkubwa wakiwa ndani ya uwanja.
“Huwa ninawaambia mara kwa mara kuwa wawapo uwanjani wanapaswa wafikirie jambo moja ambalo ni ushindi na hautaweza kupata ushindi ikiwa hautatulia katika kufanya maamuzi na kutumia akili hivyo hicho ni kitu cha kuzingatia pamoja na juhudi mazoezini.”