Home Uncategorized HAWA HAPA WAMESHIKILIA FUNGUO ZA USHINDI SIMBA V YANGA, TAIFA

HAWA HAPA WAMESHIKILIA FUNGUO ZA USHINDI SIMBA V YANGA, TAIFA


IWE jua ama mvua leo lazima mshindi apatikane Uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Yanga.
Dabi hii inabebwa na vita ya rekodi ambayo inasakwa kwani ni mara ya kwanza kwa watani hawa wa jadi kukutana kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ambalo bingwa Azam FC atakuwa mtazamaji baada ya kuvuliwa ubingwa na Simba.
Spoti Xtra inakuletea wachezaji ambao wameshikilia funguo za ushindi kwa Simba na Yanga kutokana na mchango wao walioonyesha tangu mwanzo wa michuano hii msimu huu mpaka kufika hatua ya nusu fainali hawa hapa:-
Beno Kakolanya
Mlinda mlango namba mbili  wa Simba amekuwa ni mhimili mkubwa ndani ya Simba kutinga hatua ya nusu fainali.Ikiwa imecheza mechi nne amekaa langoni mechi tatu ambazo ni dakika 270.
Amefungwa  mabao mawili huku akitoka na clean sheet moja, Desemba 12 Uwanja wa Uhuru wakati Simba ikishinda mabao 6-0 Uwanja wa Uhuru hatua ya 64 bora.
 Mbele ya Azam FC, Julai Mosi wakati Simba inashinda 2-0 Aishi Manula alikaa langoni.
Clatous Chama
Rekodi zinaonyesha amekuwa kwenye ubora kwa msimu huu licha ya kuanza kwa kusuasua. Hatua ya 64 bora Desemba 12, Uwanja wa Uhuru Simba ilishinda mabao  6-0  mbele ya Arusha FC funguo za ushindi zilikuwa miguuni mwake.
Alifunga bao moja na akatoa pasi mbili za mabao moja kwa Deo Kanda na Ibrahim Ajibu.
Francis Kahata
Hatua ya 32 bora dhidi ya Mwadui FC, Simba ilishinda mabao 2-0 alifunga bao la ushindi kwa kichwa lililoipa ushindi timu hiyo na kutinga hatua ya 16 bora.
Hassan Dilunga
Aliwachezesha namna alivyotaka Stand United ambao walikuwa imara kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Bao lake la kwanza la penalti aliyoisababisha yeye mwenyewe kwa kupiga mpira ulioishia kwenye mikono ya mchezaji wa Stand United ndani ya 18 liliwapa nguvu Simba kucheza kwa kujiamini licha ya sare ya kufungana bao 1-1 ndani ya dakika 90 Simba ilifanikiwa kupenya kwa ushindi wa penalti 3-2.
Ilikuwa Februari 25 wakati wakikutana na mbabe wao aliyewapa tabu msimu uliopita kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho, Atungo Manyundo ambaye alikuwa anakinoa kikosi cha Mashujaa wa Kigoma walioifunga Simba mabao 3-2 Uwanja wa Taifa.
Dilunga pia alifunga bao la ushindi kwa Simba huku Kakolanya akiokoa penalti moja na kuipa nafasi Simba kutinga hatua ya robo fainali.
Shomari Kapombe
Beki wa kulia mwenye uwezo wa kupandisha timu na kumwaga maji kwa guu lake la kulia.Kwenye raundi ya 16 alitoa pasi mbili za mabao kwa Clatous Chama na Francis Kahata. Aliendeleza balaa lake Uwanja wa Taifa wakati Simba ikishinda mabao 2-0 mbele ya Azam FC kwa kumpa pasi ya bao Chama.
Kwenye mchezo huo Kapombe aliumia mguu ila amesema kuwa yupo salama kwa sasa anaweza kuwa kwenye kikosi.

Mitambo iliyoshikilia ushindi kwa Yanga
Metacha Mnata
Amecheza jumla ya mechi  tatu sawa na dakika 270 na ameruhusu kufungwa bao moja ilikuwa kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Kagera Sugar. Mbele ya Gwambina na Tanzania Prisons aliweka ngome yake salama.
Farouk Shikhalo mlinda mlango namba moja wa Yanga ametumia dakika 90 kwenye mchezo dhidi ya Iringa United, Desemba 21 wakati Yanga ikishinda mabao 4-0 Uwanja wa Uhuru hatua ya 64 bora.
Patrick Sibomana
Hatua ya 64 bora, Patrick Sibomana alikuwa nyota wa mchezo ambapo wakati Yanga inashinda mabao 4-0 mbele ya Iringa United Uwanja wa Uhuru Desemba 21 alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao lililofungwa na Lamine Moro kwa kichwa.
Bernard Morrison
Kiungo huyu kipenzi cha mashabiki alishikilia ushindi kwenye mchezo wa hatua ya 32 bora dhidi ya Tanzania Prisons ambapo alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao kwa Yikpe Gnamien aliyezamisha bao kimiani kwa kichwa.
Ilikuwa ni Januari 26 Uwanja wa Taifa ambapo Morrison alipachika bao lake kwa mkwaju wa penalti iliyosababishwa na Balama Mapinduzi.
Haruna Niyonzima
Februari 22 wakati Yanga inamenyana na Gwambina FC hatua ya 16 bora bao pekee la ushindi lililoipeleka Yanga hatua ya robo fainali alilipachika akiwa nje ya 18 na mguu wa kushoto.
Gwambina ambao wanashiriki Ligi Daraja la Kwanza tayari mkononi wana tiketi ya kushiriki Ligi Kuu Bara hivyo msimu ujao wana nafasi ya kulipa kisasi kwenye mechi za ligi.
Mrisho Ngassa
Kiungo mshambuliaji, Ngassa kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali alikuwa shujaa ambapo alitoa pasi ya bao la kwanza kwa kichwa lililopachikwa kimiani na David Molinga pia alisababisha penalti iliyofungwa na Deus Kaseke iliyowapa tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali wakati wakishinda mabao 2-1 mbele ya Kagera Sugar.
SOMA NA HII  BABA LEVO AKERWA NA DIAMOND 'AMELETA UDINI'