Home Uncategorized MIONGONI MWA MATUKIO YA KUKUMBUKWA NDANI YA LIGI KUU BARA

MIONGONI MWA MATUKIO YA KUKUMBUKWA NDANI YA LIGI KUU BARA


LIGI Kuu Bara 2019/20 imefikia tamati julai 26 na sasa tunajiandaa na msimu ujao wa 2020/21 ambapo tunategemea utakuwa msimu bora zaidi ya huu ambao ulikumbwa na changamoto ya mlipuko wa virusi vya Corona.
Wakati tukianza kuusubiri kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, kuna matukio mbalimbali ambayo yalitokea msimu wa 2019/20 ambayo kwa kiasi kikubwa hayawezi kusahaulika namna hii:-
BAO KONA:
Moja ya matukio ya kustaajabisha yaliyotokea msimu huu ni tukio la bao kona, hii ilikuwa ni kwenye mchezo kati ya Yanga na Lipuli, Februari 6, Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Kwenye mchezo huu, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lipuli lakini dakika ya 52 ya mchezo, baada ya Metacha Mnata kushindwa kuudaka mpira wa David Mwasa ambao ulionekana umevuka mstari kabla kipa huyo hajaurudisha uwanjani, mwamuzi aliishangaza dunia baada ya kuamuru iwe kona. Hii ilikuwa ni kona ya ajabu zaidi kuwahi kutokea duniani. Baada ya tukio hili, waamuzi hawa walifungiwa miezi mitatu na Bodi ya Ligi.
SINGIDA UNITED WATINGA TAIFA NA DALADALA LA MAKUMBUSHO

Vibonde wa ligi msimu huu walitinga uwanjani wakitumia usafiri wa basi la abiria ‘daladala’ linalofanya safari zake kutoka Mnazi Mmoja kwenda Makumbusho kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga uliopigwa Julai 15 na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Singida walilazimika kutumia usafiri huo kutokana na basi lao kupata hitilafu wakiwa njiani kuelekea uwanjani. 

Shabiki atinga uwanjani, Yanga wasawazisha mabao yote.
Hii ilikuwa Januari 4, 2020 kwenye mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2. Ukiachana na matokeo hayo, tukio kubwa ambalo lilizua mijadala ni kitendo cha shabiki aliyevalia fulana ya njano kutinga uwanjani huku akipeperusha kitambaa chekundu hewani dakika ya 47 na baada ya tukio hilo, Yanga walisawazisha mabao yote mawili.
Kusawazishwa kwa mabao hayo kulihusishwa na tukio la shabiki huyo kuingia uwanjani na kupeperusha kitambaa hicho, tukio lililozua minong’ono ya imani za kishirikina.

YONDANI KUVAA JEZI YA LAMINE MCHEZO UKIENDELEA
Wengi tumezoea matukio ya kubadilishana jezi baina ya wachezaji kwenye mechi fulani hutokea mara baada ya mchezo kumalizika, lakini hivi karibuni kilitokea kituko cha aina yake kwenye mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya Yanga uliopigwa Julai 9, Kaitaba mkoani Kagera, ambapo beki wa Yanga, Kelvin Yondani alirudi kipindi cha pili akiwa amevalia jezi namba 25 ambayo inatumiwa na Lamine Moro.
Kitendo hicho kilifanya mwamuzi wa mchezo huo kumuamuru atoke nje kwenda kuibadilisha.
KISA GARI LA WAGONJWA, RUVU SHOOTING YAPOKONYWA POINTI
Ruvu Shooting ilijikuta ikionja joto ya jiwe baada ya kupokonywa pointi tatu na Prisons kuzawadiwa pointi hizo na mabao matatu kwenye mchezo uliokuwa upigwe Februari 11, 2020, Ruvu Shooting walikiuka kanuni zilizowekwa na Bodi ya Ligi ambayo inamtaka timu mwenyeji kuandaa gari la wagonjwa kwenye mchezo husika na endapo atashindwa basi timu pinzani itapewa pointi tatu na mabao matatu.
JPM ATINGA TAIFA SIMBA YACHAPWA
Machi 8, Yanga waliiadhibu Simba kwa bao 1-0 bao pekee lililowekwa kimiani na kiungo mtukutu Bernard Morrison kwa mpira wa adhabu. Jambo lililovuta hisia za wengi kwenye mchezo huo ni tukio la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli kutinga uwanjani hapo kushuhudia mtanange huo akiwa amevalia jezi maalum ambayo ilikuwa inawakilisha timu zote mbili.

CHENI YA KAGERE YAZUA TAFRANI
Mechi za watani huwa haziishi vituko, hii inatokana na mechi hizi kugubikwa na presha kubwa ndani na nje ya uwanja, moja ya matukio ambayo yalijitokeza kwenye mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu ni ishu ya cheni ya kinara wa mabao wa VPL, Meddie Kagere ambayo ilizua tafrani kwenye mechi ya watani iliyopigwa Machi 8.
Wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Kelvin Yondani walimvamia Kagere na kumpokonya cheni hiyo kisha kuikabidhi kwa mwamuzi wa mchezo huo Jonesia Rukyaa huku wengi wakiihusisha cheni hiyo na imani za kishirikina.
POLISI TZ, NAMUNGO WAKACHA VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO, WAPOTEZA MECHI
Kwa nyakati tofauti timu za Polisi Tanzania na Namungo FC ziligoma kutumia vyumba vya kubadilishia nguo kwenye mechi dhidi ya Simba wakihofia michezo michafu, ikiwemo kupulizwa kwa dawa za usingizi, lakini cha kustaajabisha walipoteza mechi hizo.
AMRI SAID AITOSA BIASHARA SIKU MOJA KABLA YA KUKUTANA NA SIMBA
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Biashara United ya mkoani Mara, Amri Said, ambaye kwa sasa ni kocha wa Mbeya City, aliibua mijadala baada ya kutoweka kikosini hapo huku ikiwa imebaki siku moja kabla ya kukutana na Simba.
Biashara United ilikubali kichapo cha mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Simba Septemba 29, 2019 kwenye dimba la Karume, Musoma.
SOMA NA HII  KOCHA MANCHESTER UNITED: FERNANDES BADO HAJAFIKIA KUWA RONALDO