Home Uncategorized ISHU YA USAJILI, YOUTUBE HAKUNA MCHEZAJI MBAYA, TIMU ZA BONGO ZIBADILIKE

ISHU YA USAJILI, YOUTUBE HAKUNA MCHEZAJI MBAYA, TIMU ZA BONGO ZIBADILIKE


 


DIRISHA kubwa la usajili linaendelea kushika kasi kwa sasa kila timu inataka kusajili fastafasta ili imalize ndani ya muda yaani ikifika saa 5:59 usiku ile Agosti 31, mwaka huu iwe imefanya kila kitu kinachohusiana na ishu hiyo.

 Kuna timu ambazo zinaweka wazi wachezaji ambao imewasajili na nyingine zinaficha labda kwa makusudio maalumu. Binafsi nizipongeze zile ambazo baada ya kumalizana na mchezaji zinatangaza wazi kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

 Ngoja niwaambie, klabu kuwa na ukurasa kwenye mitandao ya kijamii ni rahisi kwao kufikisha taarifa kuliko kabla hata utandawazi haujaanza.

Tumieni kurasa zenu kutangaza vitu vyenu, siku hizi kuna wadhamini pia ambao huamua kutumia mitandao kama sehemu ya kujitangaza sasa watakapoona klabu inakuwa na sehemu sahihi ya kutangaza bila ujanjaujanja inakuwa rahisi kuwavutia ili kuwekeza.

Inawezekana klabu nyingi hazifahamu hili, angalia kule Ulaya na ninatolea mfano kutoka timu za huko kwa kuwa kila mchezaji anayechipukia ndoto zake ni kucheza barani Ulaya na utaona amefollow kurasa za klabu kubwa na wachezaji wakubwa kutoka barani huko.

 

Sasa jifunzeni kutoka kwao, utaona wameajili watu maalum anaweza kuwa mpiga picha na mwandishi kwa ajili tu ya kudili na mambo yao ya online, hawa wanajua thamani ndiyo maana utaona mambo yanakwenda vizuri tu.

 

Haya nimemaliza kwenye hili la ushauri sasa twende kwenye kile nilichopanga kukizungumzia leo.

 

Tunaona usajili unavyoenda kasi kutokana na timu kupewa mwezi mmoja tu kukamilisha kila kitu na hakutakuwa na muda wa nyongeza.

 

Vita ni kubwa lakini klabu zinapaswa kutambua kama ni kweli hawa wachezaji ambao wanawasajili hususan wa kimataifa ni kweli wamewazidi uwezo wazawa?

 

Tuliona misimu mingi iliyopita ukiwemo huu wa jana tu kuna baadhi ya wachezaji wa kimataifa walisajiliwa kucheza Bongo lakini ukiangalia uwezo wao ni wamezidiwa kwa kiasi kikubwa na wazawa.

 

Ninachojua sasa hivi mawakala wanatumia nguvu kubwa kucheza michezo ambayo siyo sawa, wanatengeneza namna fulani ya kuonyesha kuwa mchezaji wake ni mkali na  thamani yake inakuwa kubwa sasa kwa kuwa klabu zetu nyingi hazina skauti hivyo huishia kupigwa tu.

SOMA NA HII  WANNE WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUCHAPISHA MAUDHUI HASI YOUTUBE

 

Klabu hamtakiwi kukaa ndani kusubiri wakala fulani awaletee mchezaji eti anakutumia na video yake akiwa uwanjani, msidanganyike nyie hakuna mchezaji mbaya Youtube.

 

Kule Youtube kila mchezaji ni mzuri na hakuna anayepoteza pasi wala kukosa mabao kizembe huyo kipa mwenyewe kila shuti anadaka tu na wakati ukifuatilia utaona pengine alifungwa mabao mawili au matatu lakini huko mtandaoni huoni kama alifungwa zaidi utaonyeshwa saves za hatari hadi huulizi mara mbili unamsajili tu.

 

Hili ni tatizo, timu zinapswa kuajili watu maalum wa kuangalia wachezaji ambao kweli wakitua wanaweza kuwa msaada, inauma kuona mgeni anakuja analipwa Sh mil 8 au 10 halafu mzawa anayetumika zaidi analipwa Sh 700,000 au mil 1 aisee hebu badilikeni.

 Kutoka Championi Jumatatu