Home Uncategorized KOCHA YANGA ATAJA ILIPOFELI KWENYE PANGA LA NYOTA 14

KOCHA YANGA ATAJA ILIPOFELI KWENYE PANGA LA NYOTA 14

 BAADA ya Klabu ya Yanga kupitisha panga na kuwaondoa kikosini zaidi ya wachezaji 14 waliokipiga na timu hiyo msimu huu, aliyekuwa kocha wa Yanga, Luc Eymael ameibuka na kusema maamuzi hayo yalikuwa na mapungufu.

Kocha huyo ambaye amefungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania ameeleza kuwa katika usajili huo yamepitishwa baadhi ya majina ya wachezaji ambao yeye aliona hawastahili kusalia huku pia kukiwa na wachezaji walioachwa ambao walipaswa kuondoka.

 

Yanga imekuwa ikikosolewa kwa maamuzi yake ya kuachana na baadhi ya wachezaji waliofanya vizuri msimu huu kama vile; David Molinga ‘Falcao’, Patrick Sibomana, Juma Abdul na Kelvin Yondani.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Eymael kutoka kwao Ubelgiji alisema kuna baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao walijitolea zaidi lakini anashangaa kwa nini wameondolewa kikosini.


“Nimepata taarifa kuwa Yanga wameachana na zaidi ya wachezaji 14, nisingependa kuliongelea sana suala hili lakini kwa mtazamo wangu nadhani maamuzi haya hayapo sahihi kwa asilimia zote.

 

“Kama ningesalia kuwa kocha wa kikosi basi naamini ningekuwa na mawazo tofauti kwani ningeendelea kubaki na baadhi ya wachezaji walioachwa na kuwaondoa waliopo kikosini hivi sasa.

 

“Tayari nimeongea na Molinga kuhusiana na suala hili lakini kama ambavyo nimesema siwezi kuingilia sana maamuzi ya watu wengine,” alisema Eymael.

SOMA NA HII  RUVU SHOOTING YAZIPIGIA HESABU OINTI TATU ZA NDANDA KESHO