KOCHA Mkuu wa Yanga, Zlatko Krmpotic amewashusha presha mashabiki wa timu yake akiwaambia mabao yatakuja, kwani kilichomuhimu kwake kwanza ni kuvuna alama tatu muhimu ili kupata hali ya kujiamini kwa wachezaji wake.
Yanga katika mechi zao tatu za awali za Ligi Kuu Bara mpaka sasa imefunga mabao matatu, huku ikiruhusu moja kwenye sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Mkapa.
Imeshinda mechi mbili mbele ya Mbeya City Uwanja wa Mkapa na mbele ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba zote ikitupia bao moja.
Kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City mtupiaji alikuwa ni beki, Lamine Moro na kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons mtupiaji alikuwa ni Michael Sarpong.
Kwa sasa kikosi kipo Dar kikiwa kimeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Mtibwa Sugar unaotarajiwa kupigwa Septemba 27, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kocha Zlatko amesema bado anataka kuona kikosi chake kinatumia zaidi nafasi wanazotengeneza uwanjani, lakini timu inaposhinda ni hatua muhimu kwa kuwa sio rahisi kupata matokeo.
“Siwezi kuridhika na kila kitu, lakini nafurahi kuona timu inashinda kwa sasa tukiwa nyumbani na hata ugenini. Sio rahisi lakini narudia hapa bado tunatengeneza timu mambo mazuri hayawezi kuja kwa haraka sana,” amesema Zlatko.