Home Uncategorized ALIYEWATUNGUA MANULA NA KAKOLANYA ATUMA UJUMBE HUU SIMBA

ALIYEWATUNGUA MANULA NA KAKOLANYA ATUMA UJUMBE HUU SIMBA

 


GERALD Mdamu, nyota mpya wa Biashara United ambaye aliibuka huko akitokea Klabu ya Mwadui FC amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Simba utakaopigwa leo Septemba 20, Uwanja wa Mkapa.


Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili kutokana na matokeo yao ya hivi karibuni kwenye mechi za ligi.


Biashara United ikiwa imecheza mechi mbili imesepa na pointi sita mazima hivyo malengo yao makubwa itakuwa ni kuendeleza rekodi yao huku Simba ikikwama mbele ya Mtibwa Sugar kusepa na pointi tatu hivyo itapambana kurejea kwenye kasi yake.

Mdamu alipokuwa ndani ya Mwadui FC aliweza kuweka rekodi ya kuwatungua makipa wote tegemeo ndani ya Simba, alianza na Aishi Manula kwenye mchezo wa ligi, Uwanja wa Kambarage wakati timu yake ya zamani ikishinda bao 1-0, kisha akamalizana na Beno Kakolanya kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho wakati timu yake ikipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.

 Mdamu amesema kuwa anatambua ubora wa makipa wote wa Simba ikiwa ni pamoja na Manula pamoja na Kakolanya hivyo akipewa nafasi ya kuanza atapambana kuwapa tabu wakiwa langoni.

“Kazi yangu ni mpira na nikiwa uwanjani ninawaza kutimiza majukumu yangu, ninajua kwamba utakuwa mchezo mgumu na wenye ushindani ila tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo kipa yoyote atakayepangwa basi nafasi tutakazopata tutazitendea haki,” alisema.

Biashara United ikiwa imetupia mabao mawili yeye ana pasi moja kibindoni aliyompa Peter Friday kwenye mchezo mbele ya Gwambina FC, Uwanja wa Karume. 

Mchezo wa leo utachezwa majira ya saa 1:00 usiku utakuwa ni wa kwanza kwa Simba kucheza ndani ya Dar kwa msimu wa 2020/21 huku kwa Biashara wao wakiwa ugenini mara ya kwanza pia.

 

SOMA NA HII  AZAM FC YASAHAU MAUMIVU YA KUPOTEZA NGAO YA JAMII, SASA NI MWENDO WA KIMATAIFA