Home Uncategorized KATI YA MORRISON, TUNOMBE,KISINDA,SARPONG, HUYU HAPA AMEWAPOTEZA WOTE

KATI YA MORRISON, TUNOMBE,KISINDA,SARPONG, HUYU HAPA AMEWAPOTEZA WOTE

 


BERNARD Morrison, kiungo mpya wa Simba ambaye amesajiliwa kwa kandarasi ya miaka miwili rekodi zinaonyesha kuwa amewafunika nyota wote waliosajiliwa ndani ya Yanga ambao ni mabosi wake wa zamani.

Kwenye usajili uliofungwa Agosti 31, Yanga ilisajili wachezaji wapya 11 miongoni mwao ikiwa ni Tuisila Kisinda ambaye ni winga sambamba na Tonombe Mukoko kiungo mkabaji wote kutoka AS Vita ya Congo, Bakari Mwamnyeto beki kutoka Coastal Union na Michael Sarpong mshambuliaji kutoka Rayorn Sport ya Rwanda.


Simba wao walisajili wachezaji saba ikiwa ni pamoja na Morrison raia wa Ghana kutoka Yanga, Larry Bwalya kiungo kutoka Klabu ya Power Dynamo ya Zambia, Cris Mugalu mshambuliaji kutoka Lusaka Dynamo na Joash Onyango beki wa kati kutoka Klabu ya Gor Mahia ya Kenya.

Licha ya kwamba Simba imecheza mechi mbili za ushindani huku Yanga ikicheza mchezo mmoja wa ushindani, Morrison amekuwa wa moto kwenye mechi zote mbili mfululizo jambo ambalo linaonyesha kwamba akiendelea na moto huo atakuwa mfalme mpya ndani ya msimu wa 2020/21.

Alianza balaa lake Agosti 22 siku ya Simba Day wakati Simba ikishinda mabao 6-0 mbele ya Vital’O ya Burundi ambapo alihusika kwenye jumla ya mabao mawili kati ya manne, alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao.

Hakupoa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 30, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, wakati Simba ikishinda mabao 2-0 mbele ya Namungo alihusika kwenye mabao yote mawili ambapo alifunga bao moja na kusababisha penalti moja iliyofungwa na John Bocco.

 Morrison amehusika kwenye jumla ya mabao manne kati ya nane yaliyofungwa na amevaa medali ya kwanza akiwa Simba na kutwaa Ngao ya Jamii na kuwapoteza nyota wote wapya.

Wengine ambao wameanza kuonyesha makeke ndani ya Simba ni pamoja na Bwalya akiwa ametoa pasi moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Vital’O na Mugalu mwenye bao bao moja mbele ya Vital’O. Onyango ambaye ni beki ameonekana kuanza kufiti kikosi cha kwanza kwa kuwa imara kuokoa hatari ambapo hajashuhudia kipa wake akiokota mpira nyavuni.

SOMA NA HII  TIMU 14 LEO KUSAKA POINTI TATU NDANI YA UWANJA

Kwa upande wa wale wa Yanga, Sarpong ambaye ni ingizo jipya aliweza kuonyesha uwezo wake ndani ya uwanja ambapo alifunga bao moja kwa kichwa na Kisinda naye alipachika bao moja kwa guu lake la kulia.

Bakari Mwamnyeto ambaye ni ingizo jipya kutoka Coastal Union ameweza kuiweka ngome salama kwenye mchezo wake wa kwanza wa kirafiki wa kimataifa ambapo timu yake ilishinda mabao 2-0. Nyota mwingine ambaye ameanza kuonyesha uwezo wake ni Tonombe ambaye ni ingizo jipya kutoka AS Vita, pacha yake na Kisinda ikijibu inaweza kuwa balaa ndani ya msimu ujao.