Home Uncategorized KCB YASAINI MKATABA WA MWAKA MMOJA KUDHAMINI LIGI KUU TANZANIA BARA

KCB YASAINI MKATABA WA MWAKA MMOJA KUDHAMINI LIGI KUU TANZANIA BARA


BENKI ya KCB leo Septemba 16, imesaini mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), kwa ajili ya kudhamini Ligi Kuu Bara, kwa mkataba wa mwaka mmoja kwa msimu wa 2020/21.


Hafla hiyo fupi imefanyika ukumbi wa Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya nne KCB kuendelea kufanya udhamini ndani ya Ligi Kuu Bara.


Christine Manyenye, Mkuu wa Idara ya Masoko wa KCB,  amesema:”Tuna furaha kubwa kwa kuingia mkataba na TFF wenye thamani ya milioni 500 na kodi ndani yake. Licha ya ugumu ambao upo kwa sasa kutokana na uwepo wa Janga la Corona ambalo limevuruga masuala ya uchumi.


“Malengo yetu ni kuona kwamba kunakuwa na ushindani ndani ya ligi pamoja na kuona kwamba kila mwanafamilia ya michezo anafurahi na ajira inapatikana kupitia michezo. 


“Pia KCB lengo letu ni kuona kwamba tunaweza kuwa sehemu ya mafanikio ya wengine pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa michezo ni ajira na tunalipa kodi,” amesema.


Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto kwa niaba ya Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kuwa sapoti inayotolewa na KCB ni kubwa na kwa kufanya hivyo ni kurudisha kwa jamii na sehemu ambayo imekuwa na mwitikio mkubwa.


“Tunaingia mwaka wa nne tukiwa na KCB, tuna uhakika kwamba hiki wanachokitoa ni kikubwa kwa ajili ya masuala ya michezo,” amesema Mguto.

SOMA NA HII  STARS YAPEWA RAI YA KUCHUKUA KIKOMBE MISRI, LAZIMA IFUATWE