Home Uncategorized UKIMFUATILIA MO DEWJI UPANDE HUU, UTAGUNDUA JAMBO TOFAUTI

UKIMFUATILIA MO DEWJI UPANDE HUU, UTAGUNDUA JAMBO TOFAUTI



Na Saleh Ally 
KUKOSOLEWA ni sehemu ya maisha ya mwanadamu ambaye anaishi akiwa amezungukwa na wanadamu ambao kawaida yao ni kuwa na mawazo tofauti. Wanadamu wakati mwingine wanaweza kukukosoa hata kwa kile wasichokijua kabisa. 


Mfano, wewe ni mtaalamu katika jambo fulani na anayekukosoa hajui lolote lakini ndio mawazo yake yanamtuma aamini anachofikiri ni kawaida. 


Bahati mbaya wako ambao hawajui lolote na kwa kuwa wana uwezo wa kuzungumza jambo, mfano kupitia mitandao ya kijamii, badala ya kuingia katika hoja wanaweza kuibuka na matusi, kitu ambacho hakiendani na hoja za msingi hata kidogo. 


Kwa mtu ambaye unabadili jambo fulani ambalo linahusisha watu, lazima usimame imara na kuendelea kusonga mbele kwa kuwa unaamini unachokifanya hakiwezi kukamilika ndani ya siku mbili, tatu au mwaka na unapopitia lazima upite katikati ya lawama, dhihaka, matusi hadi kufikia unachokihitaji. Wakati unapita huku, kwa woga huenda kuna wengi wanaweza kukukimbia hata walio karibu yako kwa hofu ya kuingia katika dhihaka, kejeli na kadhalika na wakawa mbali nawe.


Lakini siku ukifanikiwa kushinda, siku ya mwisho wataungana nawe na kushangilia pamoja. Watu wenye kariba ya kiuongozi wananielewa sana kwa mifano hii michache niliyoitoa na leo ningependa nimguse mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji maarufu kama Mo Dewji. Huyu ndugu ni shabiki wa Simba bilionea namba moja Afrika kwa wale vijana kwa mujibu wa takwimu za Forbes. 


Amekuwa shabiki wa Simba kwa miaka mingi, wenye kumbukumbu na mchezo wa soka nchini, wanaweza kuangalia picha za mwaka 2003 wakati Simba inakwenda kucheza fainali ya Kombe la Caf baada ya kuitoa Zamalek, wakiivua ubingwa wa Afrika jijini Cairo, wakati huo ikiwa ndio timu bora Afrika. Mo Dewji alikuwa kati ya Wanasimba walioshiriki wakiungana na wadau wengine, kiongozi akiwa ni Azim Dewji. 


Hii ni kuonyesha Simba yeye si mgeni, lakini ndoto yake imekwenda mbali hadi aliporejea. Kauli kadhaa za Dewji ndio zimenifanya kuangalia ndani zaidi, mojawapo ni ile ya “Siondoki Simba ng’o” akisisitiza kuna watu wanataka kumchanganya ili ajitoe na kuwafanya wengi wanaomuamini waanze kuumia kutokana na kufeli kwa Simba lakini ile kauli ya hata watu wa familia yake, wako wanaomshangaa kuona vipi aendelee na Simba kwa kuwa Simba sasa wala haiingizi faida. 


Mo Dewji anaamini Simba itaanza kuingiza faida baada ya angalau miaka 10 ijayo. Lakini anaona kuna neema inakuja, ndio maana ameendelea kupambana. Ukiangalia ndani ya misimu minne, bajeti ya Simba imetoka Sh milioni 560 kwa mwaka hadi takriban bilioni 7, zaidi ya mara 10. 


Kupaa kwa bajeti kunaonyesha kuwa Simba inapiga hatua kwenda katika ukubwa. Kwa kuwa kila unapolazimika kujitanua kwa bajeti, maana yake unakua na unalazimika kuwa na mipango thabiti kushikilia ulipo na uendelee kukua. Kubaki hapo lazima uwe na watu wa uhakika, wafanyabiashara wanaotambua nini maana ya kusonga mbele, si kazi ndogo, Mo Dewji kajitahidi sana katika hili. Ubingwa mara tatu: Simba ndio timu mfano na yenye mafanikio makubwa zaidi katika miaka minne na kumbuka, iko chini ya Mo Dewji. 


Mafanikio haya, lazima uingie ndani na kufanya utafiti, hayawezi kuwa yameshikiliwa na nguzo za miti mikavu, lazima ni nondo imara kwa maana ya watu wenye maono jenga na mawazo chanya yenye hesabu sahihi. Mfano: Ukisikia mtu anakuambia Simba si mfano kwa kila timu ya Tanzania na Afrika Mashariki yote, atakuwa na roho mbaya au moyo wa kutotaka kujifunza.


Angalia, kila timu leo imelazimika kuzindua jezi kama Simba, kila timu inatamani au imefanya tamasha linalofanana na Simba na hata watani wao Yanga ambao ni wakongwe wenzao, wamekopi karibu kila kitu kilichofanywa na watani wao. Ukiangalia tofauti kati ya Yanga na Simba katika matamasha yao, utagundua Yanga waliwavalisha wachezaji wao suti.


Zaidi ya hapo unaona mambo yalienda sawa na hili si jambo baya kuigana lakini vizuri kuongeza ubunifu. Suala la kushindana mashabiki kwa promosheni, Simba wameanzisha kwa mfumo ambao leo unazivutia klabu nyingi za Tanzania lakini Afrika Mashariki na hata baadhi ya nchi nyingine za Afrika. Unaona kwa ukanda wetu kwa sasa, Simba ndio timu inayotajwa sana. Hii ni kutokana na kuwa na mifumo bora ya uendeshaji inayoifanya kuimarika siku hadi siku. 


Kwangu ukiachana na yale maneno ya Sh bilioni 20 ataweka lini, namchungulia Mo Dewji upande huu wa pili kwamba, hastahili lawama pekee na badala yake kuna mambo ambayo amefanya ambayo tunapaswa kuyaona na kuyasema kwa uzuri. Ukichungulia vizuri, unagundua kuwa kweli kutokana na kuunda mifumo thabiri na watu sahihi waliojenga timu ya kusaka maendeleo, kuna jambo bora kalijenga ambalo leo limegeuka kuwa chachu ya mabadiliko na kufanya kuwe na hamu ya maendeleo na mabadiliko kwa Yanga, Azam FC na kadhalika lakini pia kwa majirani zetu. 


Mtu huyu, hapaswi kupondwa mawe tu. Badala yake, uhuru wa kukosoa tunaweza kuutumia vizuri kuhoji lakini baada ya kuwa tumepata uhakika wa jambo tunalohoji kwa kuwa hata kuhoji kunajenga pia lakini kusiwe kule kwa lengo la ubinafsi. Wakati wa kwenda kwenye mabadiliko ya jambo fulani, makosa hayawezi kukosekana kwa mwanadamu hata ungekuwa wewe, basi tupongeze na kukosoa ili tujenge na si kukosoa tu, halafu tukosoe tena, halafu tukosea tena.
SOMA NA HII  NAMUNGO WATUSUA KIMATAIFA,NGOMA UGENINI YAWA 3-3