Home Uncategorized RUVU SHOOTING: KUHAMIA UHURU KUMETUONGEZEA GHARAMA, MASHABIKI HAWAJI

RUVU SHOOTING: KUHAMIA UHURU KUMETUONGEZEA GHARAMA, MASHABIKI HAWAJI


 TIMU ya Ruvu Shooting yenye maskani yake Pwani, imesema kuwa kufungiwa kwa Uwanja wa Mabatini na Bodi ya Ligi Tanzania, (TPLB) ili ufanyiwe maboresho umewaponza kwenye suala la mapato kwa kuwa mashabiki wengi wanashindwa kufika Uwanja wa Uhuru.

Uwanja wa Mabatini ambao unatumiwa na Ruvu Shooting kwa mechi za nyumbani ulifungwa na TBLB, Septemba 25 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosa baadhi ya sifa za kikanuni kama zilivyoainishwa kwenye kanuni ya saba inayozungumzia uwanja na sheria namba moja ya mpira wa miguu, inayozungumzia  uwanja.

Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema kuwa mashabiki wengi kwa sasa wanakosa fursa ya kuitazama timu hiyo ikiwa inacheza nyumbani kwa sababu wanashidwa kusafiri kutoka Mlandizi mpaka Dar kutokana na changamoto mbalimbali.

“Mashabiki wanakosa fursa ya kuangalia timu yao ikiwa nyumbani kwakuwa sio wote wenye uwezo wa kusafiri kwenda kutizama mechi za Ruvu wakiwa wanacheza uwanja wa Uhuru jambo ambalo linatukosesha mapato.

“ Changamoto nyingine naweza kusema ni kwamba gharama za uendeshaji kila tuendapo Uhuru. Gharama za usafiri, chakula, kulala huongezeka wakati wa kwenda kucheza kwenye uwanja huo.

“Hizi ndizo sababu tunapambana kuwa tunaporudi kutoka Dodoma uwanja wetu tayari uwe umeshafanyiwa marekebisho na umekamilika kwa maelekezo tuliyopewa na Bodi ya ligi kuhakikisha kuwa tunakwenda sawasawa.


“Tulipokuwa Uwanja wa Mabatini pale wachezaji walikuwa wanapata kila kitu kuanzia msosi mzuri kutoka kwa wapishi wetu wenyewe sasa mambo yanapobadilika kuna mambo mengine yanaongezeka,” amesema.


Ruvu Shooting mchezo wake wa raundi ya tano itakuwa ni dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

 

SOMA NA HII  SURE BOY WA AZAM FC AINGIA ANGA ZA YANGA