SVEN Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa wachezaji wake wanazidi kuimarika kila siku hivyo anaamini kwamba atapata pointi tatu kwenye mechi zake zinazofuata.
Kwa sasa Simba iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne ina kibarua cha kumenyana na JKT Tanzania, Oktoba 4, Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Mchezo wake wa raundi ya nne Simba imetoka kushinda kwa mabao 3-0 mbele ya Gwambina FC inakwenda Dodoma kukutana na JKT Tanzania ambayo imetoka kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 mbele ya Coastal Union.
Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa 2019/20 timu hizo zilipokutana mara mbili kwenye pointi sita zote ziligawana pointi tatutatu ambao mchezo wa kwanza Simba ilishinda mabao 3-1 na ule wa mzunguko wa pili JKT Tanzania ilishinda bao 1-0.
Svev amesema:”Wachezaji wanazidi kuwa bora na imara, kila baada ya mechi tunafanyia kazi mapungufu ili kuona namna gani wataweza kuwa imara zaidi.
“Kwenye safu ya ushambuliaji tatizo kubwa ni kwenye umaliziaji wa nafasi ambazo tunatengeneza hivyo hilo tunalifanyia kazi kwa sasa.”
Kikosi kinatarajiwa kuondoka kesho kuelekea Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo na kikimalizana na JKT Tanzania kitarejea Bongo, Uwanja wa Mkapa Oktoba 18 kumenyana na watani zake wa jadi Yanga.