Home Uncategorized HIZI PACHA ZA KAZI, ZITASUMBUA OKTOBA 18 KWENYE DABI

HIZI PACHA ZA KAZI, ZITASUMBUA OKTOBA 18 KWENYE DABI

 


JOTO la mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba taratibu linazidi kupanda kwa sasa ambapo kila timu imeanza kutengeneza silaha zao za kazi kabla ya kukutana kwa watani hawa wa jadi.

Zimebaki siku 14 kwa sasa kabla ya watani hawa kukutana ambapo Yanga watakuwa wenyeji kwenye mchezo huu wa kwanza kwa msimu wa 2020/21.

Mechi zao za msimu uliopita mashujaa ni Yanga kwa kuwa mchezo wa kwanza ambapo Simba walikuwa wenyeji, Januari 4 walitoshana nguvu kwa sare ya kufungana mabao 2-2 ila ile ya Machi 8 wakati Yanga wakiwa wenyeji wa mchezo Simba ilitunguliwa bao 1-0.

Hizi hapa pacha mbili ambazo zimeanza kupikwa kabla ya Oktoba 18 namna hii:-

Sarpong v Nchimbi

Pacha hii ilianza kujibu kwenye mchezo wa kwanza wa nyota hawa walipocheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Aigle Noir uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Agosti 30.

Wakati  Michael Sarpong akipachika bao lake la kwanza kwa kichwa kwenye ardhi ya Bongo alitumia pasi Ditram Nchimbi. Uzoefu wa Nchimbi kucheza dabi unampa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza mbele ya Simba, Oktoba 18.

Sarpong ametumia jumla ya dakika 426 kwenye mechi zake ilikuwa dakika 68 mbele ya Aigle Noir,dakika 90 mbele ya Tanzania Prisons, Septemba 6 ,alifunga bao lake la kwanza kwenye ligi, mbele ya Mbeya City dakika 90, Septemba 13 na mechi dhidi ya Kagera Sugar, Septemba 19 alitumia dakika 88 wakati Yanga ikishinda bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar Septemba 27.

 Nchimbi ametumia jumla dakika 166 ilikua dakika 53 mbele ya Aigle Noir wakati pacha yao ikijibu. Dakika 90 mbele ya Tanzania Prisons, dakika 21 mbele ya Mbeya City na dakika 2 mbele ya Mtibwa Sugar.

Tonombe v Kisinda

Hawa wote wametoka timu moja ya AS Vita ya Congo, Tonombe Mukoko na Tuisila Kisinda wamekuwa na maelewano ndani ya uwanja wakianza pamoja.

Pacha yao iliibukia Bukoba wakati Yanga ikishinda bao 1-0 mbele ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba. Kisinda alitengeneza pasi mpenyezo kwa Tonombe ambaye alifunga bao lake la kwanza ndani ya ligi.

Tonombe alitumia dakika 285 ndani ya ligi ambapo alitumia 15 mbele ya Tanzania Prisons, dakika 90 mbele ya Mbeya City, dakika 90 mbele ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar 90.

Kisinda ametumia dakika 315 ndani ya ligi ikiwa dakika 45 mbele ya Tanzania Prisons, mbele ya Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar aliyeyusha dakika zote 90.

Lamine v Carinhos

Pacha ambayo inasubiriwa na mashabiki wa Yanga kuona namna gani inaweza kujibu kwenye dabi ikiwa Carlos Carinhos raia wa Angola mara yake ya kwanza kucheza dabi.Lamine yeye ana uzoefu kwani msimu uliopita alikuwa ndani ya kikosi cha Yanga.

Wote wawili wamekuwa na maelewano mazuri ambapo Yanga ikiwa imefunga mabao manne wamehusika kwenye mabao mawili, Lamine amefunga mabao mawili na Carinhos ametoa pasi mbili za mabao kwa mipira ya kona ambayo ilikutana na Lamine.

SOMA NA HII  NAMUNGO FC: TATIZO LIPO KWENYE MAANDALIZI

Lamine ametumia dakika 270 ambapo amecheza mechi tatu mbele ya Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar na Carinhos alitumia jumla ya dakika 137 ndani ya ligi, dakika 30 mbele ya Mbeya City,35 mbele ya Kagera Sugar na 72 mbele ya Mtibwa Sugar.

Luis v Kagere

Nyota hawa wamekuwa na pacha matata ambayo imekuwa ikijibu kila wawapo ndani ya uwanja. Kagere ametupia jumla ya mabao mawili na mpishi wa pasi hizo ni Luis Miqussone.

Ilikuwa ni mbele ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 4-0 na mbele ya Gwambina FC wakati Simba ikishinda mabao 3-0 alimpa pasi moja Kagere.

Luis ametumia dakika 270 kwenye mechi zake tatu ilikuwa ni mbele ya Mtibwa Sugar, Bashara United na Gwambina na Kagere ametumia jumla ya dakika 197 ilikuwa dakika 23 mbele ya Ihefu,24 mbele ya Mtibwa Sugar,76 mbele ya Biashara United na 74 mbele ya Gwambina.

Chama v Mugalu

Kiungo bora wa msimu wa 2019/20 Clatous Chama bado ameendelea kuwa kwenye ubora wake na kwa msimu wa 2020/21 ametoa jumla ya pasi mbili na kufunga mabao mawili.Chris Mugalu ambaye ni ingizo jipya ndani ya Simba alifanikiwa kupachika bao lake la kwanza kwenye ligi akitumia pasi ya kisigino ya Chama.

Ilikuwa Uwanja wa Mkapa mbele ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 4-0.

Chama ametumia jumla dakika 356 ndani ya ligi ilikuwa 90 mbele ya Ihefu, 90 mbele ya Mtibwa Sugar na 90 mbele ya Biashara United na ametumia dakika 86 mbele ya Gwambina. Mugalu ametumia dakika 14 mbele ya Biashara United na dakika 16 mbele ya Gwambina FC na kumfanya atumie dakika 30.

Mzamiru v Bocco

Mzamiru Yassin ni miongoni mwa wazawa ambao huanza kwa kasi kisha kupotea jumlajumla. Msimu uliopita kwenye mechi mbili za mwanzo msimu wa 2019/20 alitoa pasi tatu za mabao ila msimu huu kwenye mechi mbili za mwanzo ametoa pasi moja ya bao na kufunga mabao mawili.

Wakati Simba ikishinda mabao 2-1 mbele ya Ihefu alimpa pasi nahodha John Bocco aliyefungua akaunti yake ya mabao kwa msimu wa 2020/21 Uwanja wa Sokoine. Pacha hii ni miongoni mwa zile ambazo zikipewa nafasi Oktoba 18 patakuwa hapatoshi.

Bocco ametumia dakika 180 ilikuwa ni mbele ya Ihefu dakika 90  na Mtibwa Sugar dakika 90 na Mzamiru ametumia jumla ya dakika 347 kwenye ligi ilitumia dakika 90 mbele ya Ihefu,Biashara United dakika 90, Gwambina dakika 90 na ametumia dakika 77 mbele ya Mtibwa Sugar.